Serikali na mikakati kumaliza changamoto tasnia ya mbolea

Imeelezwa kwamba baada ya serikali kukutana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea kulikosababishwa na kupanda kwa bidhaa hiyo kwenye soko la dunia, Serikali imekuja na mikakati kabambe kukabiliana na changamoto hiyo.
Mosi ni kuielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha
inatoa bei elekezi ya mbolea kupelekea bei ya bidhaa hiyo kutopandishwa kiholela, kutenga bajeti kwa ajili ya ruzuku ili kuwapunguzia wakulima gharama za bidhaa hiyo pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea vya ndani.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde tarehe 26 June, 2022 wakati wa ziara ya wabunge wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini iliyolenga kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa katika eneo la Nala jijini Dodoma.
Mavunde alisema serikali inatambua kwamba mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndiyo inayotegemewa zaidi nchini kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara na kuona ni vyema kwa wabunge hao kutembelea kiwanda hicho ili kujionea uwekezaji mubwa unaofanywa katika tasnia ya mbolea.
Mavunde alieleza kuwa, uwekezaji huo unaofanywa na mwekezaji kutoka nchini Burundi ni matokeo ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Samia Suluhu Hassan nchini Burundi na kueleza fursa ya uwekezaji katika eneo hilo.
Alisema uwekezaji huo ni moja ya mikakati ya serikali kuhakikisha changamoto ya bei ya mbolea ambayo ni kilio cha wakulima nchini inafikia ukomo mara baada ya uzalishaji unaotarajiwa kuanza ifkapo Julai 2022.
“Kabla ya kuanza uzalishaji tayari serikali ilishatoa maelekezo kwa
taasisi zake husika kwenda kufanya tafiti, ikiwemo kuangalia aina ya udongo katika mikoa mbalimbali hapa nchini ili kubaini kiwango cha mbolea aina ya Organo Mineral itakayozalishwa kiwandani hapo kuwa na tija kwa wakulima wa aina zote za udongo.
Naibu Waziri aliwaomba wabunge hao kupeleka ujumbe kwa wakulima katika majimbo yao pamoja na kuueleza umma jitihada zinazofanywa na serikali katika kukabiliana na changamoto ya bei na upatikanaji wa mbolea nchini.
Naye Mwenyeki wa muda wa Wabunge kutoka Nyanda za Juu Kusini, Jackson Chimwaga aliishkuru serikali kutokana na jitihada za kutatua changamoto ya upatikanaji na bei ya mbolea kwa kuhamasisha uwekezaji wa kiwanda hicho unaofanyika nchini.
Chimaga alisema, kama kiwanda hicho kitakachokuwa kikizalisha mbolea ya asili, kitakuwa na faida kubwa kwa wakulima kutokana na kwamba itaongeza uzalishaji na kutunza rutuba ya udongo.
Alisema wao kama Wabunge wa Nyanda hizo, watakwenda kuwa mabalozi wazuri wa mbolea inayozalishwa kiwandani hapo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Nduwimana Nazaire
aliwashkuru wabunge kwa kutenga muda wa kuwatembelea na kujionea uwekezaji unavyofanyika kiwandani hapo huku akishukuru kwa ushirikiano wanaoupata kutoka serikali ya Tanzania na kuahidi kutoiangusha serikali kwa kuzalisha mbolea itakayoleta
matokeo chanya.
Kufuatia moja ya malighafi zitakazotumika kiwanda hapo kuwa ni samadi Mkurugenzi wa kiwanda hicho alisema mahitaji ya Samadi katika hatua ya awali ya uwekezaji ni tani
117,000.
Alieleza kuwa, tayari ofisi yake imeandaa vituo kwa ajili ya kukusanyia samadi hiyo na kubainisha kuwa wafugaji watapata fursa ya kujipatia kipato kupitia mbolea aina ya samadi itakayotumika katika uzalishaji wa organic fertilizer kiwandani hapo.
Mwisho.