Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Ruzuku ya mbolea yachangia ongezeko uzalishaji wa mazao ya chakula
04 Jun, 2024
Ruzuku ya mbolea yachangia ongezeko uzalishaji wa mazao ya chakula

Ruzuku ya mbolea yachangia ongezeko uzalishaji wa mazao ya chakula

  1. Mpango wa ruzuku kutekelezwa hadi  mwaka 2025/2026

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameeleza kuwa, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 uliongezeka na kufikia tani 20,402,014 ikilinganishwa na tani 17,148,290 katika msimu wa kilimo wa 2021/2022.

Alisema, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 19 katika kipindi tajwa ambapo uzalishaji wa mazao ya nafaka ulikuwa ni tani 11,448,757 ikilinganishwa na tani 9,233,298 msimu wa kilimo 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 23.9 na uzalishaji wa mazao yasiyo nafaka ulikuwa tani 8,953,258 ikilinganishwa na tani 7,914,992 katika msimu wa kilimo 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 13.1.

Waziri Bashe alieleza hayo wakati akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za wizara ya kilimo kwa mwaka 2024/2025 mnamo tarehe 2 Mei, 2024.

Alisema, uzalishaji wa chakula kwa msimu wa kilimo wa 2022/2023 ulitosheleza mahitaji ya chakula ya tani 16,390,404 kwa mwaka 2023/2024 na kuwepo kwa ziada ya tani 4,011,611 na hivyo, Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124 ikilinganishwa na utoshelevu wa asilimia 114 mwaka 2022/2023.

Waziri Bashe alieleza kuwa pamoja na uwepo wa sababu nyingine zilizopelekea ongezeko hilo ni upatikanaji wa mbolea inayotolewa kwa wakulima kwa ruzuku.

Alisema, hadi kufikia mwezi Aprili, 2024 upatikanaji wa mbolea umefikia tani 1,052,218.4 ikilinganishwa na tani 819,442 mwaka 2022/2023 sawa na asilimia 123.95 ya makadirio ya mahitaji ya mbolea ya tani 848,884 kwa mwaka.

Aidha, Waziri Bashe alibainisha kuwa, tani 471,839.9 zenye thamani ya ruzuku ya Shilingi 136,495,898,332 zimesambazwa kwa wakulima kupitia mpango wa ruzuku ambapo tani 92,134.65 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 13.7 zimetolewa kama ruzuku kwenye zao la tumbaku.

Ameongeza kuwa, ili kurahisisha usambazaji wa mbolea kwa wakulima nchini, Wizara ya Kilimo imeongeza idadi ya waingizaji wakubwa wa mbolea kutoka 28 mwaka 2022/2023 hadi 31 mwaka 2023/2024; mawakala wadogo 3,265 mwaka 2022/2023 hadi 3,500 mwaka 2023/2024; na kusajili vyama vya ushirika 776 kwa ajili ya kuwa mawakala wa kusambaza mbolea za ruzuku kwa wakulima.

Vilevile Waziri Bashe alisema, ili kuwa na uhakika wa takwimu na taarifa za wakulima zitakazoiwezesha Serikali kuwa na mipango sahihi ya kuendeleza kilimo nchini; Wizara kupitia TFRA imepanga kuendelea na usajili wa wakulima katika mfumo wa kidigiti; kutoa mafunzo ya ukaguzi wa ubora wa mbolea; kusajili aina mpya za mbolea na visaidizi vyake 85; na kutoa leseni 2,100 za biashara ya mbolea.

Alisema hadi Aprili, 2024 wakulima 3,910,556 wamesajiliwa kwenye kanzidata https://ruzuku.tfra.go.tz na kueleza usajili huo utakamilika kwa kuchukua majira nukta (coordinates (GPS) za mashamba ya wakulima wadogo na baadaye mkulima kupatiwa hati ya shamba lake.

Waziri Bashe alibainisha kuwa, kwa mwaka 2024/2025 Wizara itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na viuatilifu kupitia mpango wa ruzuku kwa mazao yote na kubainisha kuwa kupitia TFRA, Serikali itaratibu uingizwaji wa tani 1,086,115 za mbolea na kuzisambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku utakaoendelea hadi mwaka 2025/2026.

Pia alisema Wizara itakamilisha vigezo muhimu katika mfumo wa usajili wa wakulima huku ikisajili wakulima, waagizaji na wasambazaji wa mbolea katika mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kuimarisha usambazaji wa mbolea nchini.

Akizungumza kuhusu Kampuni la Mbolea Tanzania (TFC) alisema itanunua tani 100,000 za mbolea na kusambaza kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku.

Pamoja na hayo, TFC kwa kushirikiana na Kampuni ya Serikali ya Morocco (OCP Group Africa) itajenga kiwanda cha kuchanganya mbolea (Bulk Blending Facilities) chenye uwezo wa kuchanganya tani 120 za mbolea kwa saa kitakachochanganya mbolea kwa kuzingatia afya ya udongo ya eneo husika na hivyo wakulima kupata mbolea kuingana na mahitaji ya udongo.

Alisema, ili kuwezesha upatikanaji wa mbolea kwa wakulima karibu na maeneo yao na kwa wakati, kwa mwaka 2024/2025 Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na TFRA itaendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika kuwa Mawakala wa kusambaza mbolea kwa mpango wa ruzuku.

Waziri Bashe aliliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha shilingi 1,248,961,680,000 kupitia Fungu 43, Fungu 05 na Fungu 24 ikiwa ni bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka 2024/2025.