Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Ruzuku ya mbolea kuongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima Tabora
29 May, 2024
Ruzuku ya mbolea kuongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima Tabora

Imeelezwa kuwa, kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima na vitendea kazi kwa maafisa ugani, uzalishaji wa zao la tumbaku umeongezeka kutoka kilo 29,815,082 mwaka 2021/2022 hadi kilo 62,964,460.83 mwaka 2022/2023.



Aidha, bei ya wastani imeongezeka kutoka Dola za Marekani 1.81 kwa kilo hadi kufikia Dola 2.3 katika kipindi hicho na kueleza ongezeko hilo ni sawa na asilimia 111 na asilimia 27 mtawalia.



Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Simon Chacha alipokuwa akihutubia hadhira kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yalifanyika katika viwanja vya Chipukizi vilivyopo Manispaa ya Tabora.



Mkuu wa Wilaya Chacha amesema, mapato ya wakulima katika kipindi hicho yameongezeka kutoka Dola za Marekani 54,017,356.88 hadi kufikia Dola 144,732,352.99 sawa na ongezeko la asilimia 168.



Pamoja na hayo Chaha amesema, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023, Mkoa wa Tabora ulizalisha jumla ya tani 1,153,654 ya mazao mchanganyiko ya chakula ikiwa ni Mazao ya wanga na jamii ya kunde.



Amesema, uzalishaji huo umeongezeka ukilinganisha na uzalishaji wa mwaka 2021/2022 ambapo jumla ya tani 973,106 ya mazao mchanganyiko ya chakula zilizalishwa.



Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuendelea kufikisha elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwani itasaidia katika kuongeza tija kwa wakulima.



Pia, ametoa maelekezo kwa Wenyeviti wa Kamati za Pembejeo za Wilaya (Wakuu wa Wilaya) kuhakikisha wakulima wote wanajiandikisha na wale waliojiandikisha msimu uliopita wa kilimo wanauhisha taarifa zao ili waweze kunufaika na mbolea ya ruzuku.



Pili, amewataka kuhakikisha wanadhibiti tabia ya baadhi ya watendaji kutotoa ushirikiano kwa wakulima wakati wa usajili na kueleza hali hiyo haikubaliki na ikibainika mtendaji anazuia wakulima kujisajili hatua kali zichukuliwe dhidi yao kwa kukwamisha mpango huu muhimu wa kitaifa.



Amewataka kufanya mapitio ya bei elekezi za mbolea zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na kuzifanyia marekebisho endapo zitaonekana haziakisi uhalisia wa kijiografia na miundombinu ya eneo husika na taarifa yenye marekebisho kuwasilisha TFRA na maelekezo mengine yatakayowafanya wakulima kunufaika na mbolea za ruzuku.



Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhani Kapera akitoa salamu za Mwenyekiti wa CCM ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA na Menejimenti yao kwa utendaji mzuri na kueleza hayo ni matokeo mazuri ya Mwenyekiti wa bodi mahiri katika masuala ya kisiasa na biashara Dkt. Anthony Diallo.



Ametoa ombi la TFRA kuendelea kuboresha mfu o wa mbolea za ruzuku ili kupunguza changamoto zilizojitokeza msimu uliopita wa kilimo na kueleza wana imani kubwa kuwa changamoto hazitajirudia.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TFRA. Dkt. Anthony Diallo aliwashukuru wadau wote kwa kujitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo yatakayofikia kilele Ijumaa tarehe 13 Oktoba, 2023 na kutoa wito kwa wakulima na wananchi wote kutembelea maonesho hayo ili kujifunza elimu ya mbolea pamoja na masuala mengine muhimu kama vile matumizi ya mbegu bora, viuatilifu na namna ya kupata mikopo ili kuendesha shughuli zao za kilimo.