Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Rais Samia kuzindua mpango utoaji mbolea ya ruzuku
29 May, 2024
Rais Samia kuzindua mpango utoaji mbolea ya ruzuku

Imeelezwa kwamba mpango wa utoaji ruzuku ya mbolea kwa wakulima utazinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan siku ya kilele cha Maonyesho ya Wakulima maarufu Nanenane tarehe 8.8.2022 yatakayofanyika kitaifa mkoani Mbeya.


Hayo yameelezwa leo tarehe 26 Julai, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA). Dkt. Stephan Ngailo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vetenari J ijini Dar es Salaam.


Amesema, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (Mb), alizindua Mwongozo wa Utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku pamoja na usajili wa wakulima tarehe 4 Julai, 2022 katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa ruzuku.


Kufuatia uzinduzi huo, wakulima wote nchini wanahimizwa kujitokeza kujiandikisha katika Serikali za Vijiji vyao ili waweze kunufaika na mpango wa Serikali wa kuwapunguzia makali ya bei ya mbolea kupitia ruzuku hiyo.


Akizungumzia wahusika katika utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya mbolea, Dkt Ngailo alisema mchakato utahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kilimo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kamati Tendaji ya Ruzuku, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Waingizaji/Wazalishaji wa Mbolea, Mawakala (Agrodealers) wa Mbolea, Taasisi za Fedha, Wakulima na wadau wengine muhimu kwenye Sekta ya Kilimo.


Akitoa wito kwa wakulima na wadau wa mbolea kujisajili, Dkt Ngailo amesema uzoefu unaonesha utekelezaji wa mipango ya ruzuku kwa miaka iliyopita iligubikwa na mianya mingi ya udanganyifu na hivyo Serikali imeamua kutumia mfumo wa kidijitali kutekeleza mpango wa ruzuku kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 ili kuongeza ufanisi, kupunguza mianya ya udanganyifu, muda na gharama za usimamizi wa ruzuku husika.


Pamoja na aina nyingine za mbolea zitakazohusika kwenye ruzuku ya mbolea ikiwa ni pamoja na mbolea zinazozalishwa na viwanda vya ndani kwa kuzingatia mahitaji ya soko, Dkt. Ngailo amesema, Mbolea zitakazohusika kwenye ruzuku ni DAP ikiwa ni mbolea ya kupandia na Urea kwa ajili ya kukuzia ambazo ni takribani 50% ya matumizi ya mbolea nchini.