Rais Samia awataka wafanyakazi kuzingatia utu na staha kazini
Rais Samia awataka wafanyakazi kuzingatia utu na staha kazini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, amewahimiza wafanyakazi nchini kuzingatia utu, staha na uwajibikaji kazini ili kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya taifa.
Rais Samia alitoa wito huo leo, Ijumaa, Mei 1, 2026, alipokuwa akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,” Rais Samia amesema kuwa kazi si chanzo cha kipato pekee, bali ni msingi wa heshima, utu na maendeleo ya taifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kazi zenye staha zinazolinda hadhi ya mfanyakazi, ikiwemo usalama kazini, kipato cha haki na mazingira bora ya kazi.
Kwa upande wake mfanyakazi Bora wa TFRA,Elizabeth Bolle, Meneja wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, ameishukuru Menejimenti ya TFRA kwa imani na ushirikiano waliompa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha Bolle amesema,anathamini kwa dhati mchango wa kila mjumbe wa Menejimenti na watumishi wote kwa ujumla, akibainisha kuwa mafanikio yake yametokana na kazi ya pamoja.
Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi, ambapo wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) walishiriki kikamilifu kuadhimisha mchango wao katika maendeleo ya taifa.
