Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
MIAKA MINNE YA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN YAPANDISHA BIASHARA YA MBOLEA NCHINI
19 Mar, 2025
MIAKA MINNE YA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN YAPANDISHA BIASHARA YA MBOLEA NCHINI
  • Wafanyabiashara wa mbolea nchini waongezeka
  • Huduma za udhibiti zaimarishwa kufuatia ujenzi wa maabara ya mbolea
  • Wakulima kurahisishiwa huduma kwa kupewa kadi Janja

Biashara ya mbolea nchini imeelezwa kukua kwa kiasi kikubwa ambapo wafanyabiashara wa mbolea waliopewa leseni wameongezeka kutoka 3,069 mwaka 2020/21 hadi 7,302 Februari, 2025 huku upatikanaji wa mbolea uikiongezeka kutoka tani 766,024 mwaka 2020/2021 hadi tani 1,213,729 mwaka 2023/2024.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 19 machi, 2025 jijini Dodoma.

Bw. Joel ameeleza kuwa uingizaji wa mbolea umeongezeka kutoka tani 504,122 mwaka 2020/2021 hadi tani 728,758 mwaka 2023/2024 na uzalishaji wa ndani umeongezeka kutoka tani 42,695 mwaka 2020/2021 hadi tani 158,628 mwaka 2023/2024.

Akielezea kuhusu Mpango wa Ruzuku ya Mbolea, Bw. Joel amesema eneo hilo limekuwa moja ya mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo kwa kupitia mpango huo uliopunguza gharama ya mbolea kwa wakulima umewafanya wakulima kununua mbolea kwa bei ya kuanzia shilingi 40,000/= hadi 80,000/= kwa kutegemea aina ya mbolea, zao na umbali aliko mkulima kutoka kwenye chanzo ikiwa ni sawa na punguzo la takribani asilimia 50 ya bei halisi.

“Kabla ya kuanza utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea katika msimu wa 2021/2022, Sekta ya Kilimo ilikabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la ndani kutokana na kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia” ameeleza Bw. Joel.

Aidha, Bw. Joel amesema matumizi ya mbolea nchini yameongezeka kutoka tani 363,599 mwaka 2020/2021 hadi tani 840,714 mwaka 2023/2024 ambapo ongezeko hilo limewezesha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 za virutubisho kwa hekta mwaka 2020/2021 hadi kilo 24 za virutubisho kwa hekta mwaka 2024/2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent amesema katika kipindi cha miaka minne cha Uongozi wa Awamu ya Sita, Serikali kwa mara ya kwanza imeandaa Mkakati wa Taifa wa Mbolea na Afya ya Udongo (2024 - 2030) ambao tayari umeanza kutumika.

Pamoja na hayo, Bw. Joel ameeeleza kuwa Mamlaka hiyo imeanzisha Maabara ya kisasa ya kupima sampuli za mbolea, udongo na tishu za mimea hivyo kuwahakikishia walaji ubora wa bidhaa na mazao yatokanayo na matumizi ya pembejeo hizo.

Akielezea kuhusu uboreshaji wa utendaji kazi, Joel amesema Mamlaka imeimarisha matumizi ya TEHAMA yaliyopunguza muda na gharama za kupata huduma kwa wateja Vilevile, matumizi ya mifumo yamewezesha upatikanaji wa takwimu za uhakika zinazoiwezesha Serikali kuweka mipango ya kuendeleza tasnia ya mbolea na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.

"kupitia Mfumo wa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo (Agricultural Inputs Subsidy System), wakulima wanaendelea kupata fursa ya kuingizwa kwenye mifumo rasmi ya kifedha kupitia Kadi Janja na fursa ya kupata Hati Miliki za mashamba, uwezeshaji wa huduma za kibenki pamoja na huduma nyigine muhimu." ameeleza Bw Joel.

Sambamba na hayo ameeleza kuwa, katika kutambua umuhimu wa Sekta ya Kilimo nchini na kuhakikisha pembejeo za mbolea zinapatikana na kumfikia mkulima kwa wakati na kwa gharama himilivu, Mhe. Rais ameelekeza bandari ya Tanga iweze kutumika kuhudumia meli zinazoingiza mbolea nchini na zinazosafirishwa kwenda nchi jirani.

Akihitimisha hotuba yake, Joel ametoa rai kwa wakulima nchini kuendelea kujisajili ili waendelee kunufaika na utekelezaji wa mpango wa mbolea za ruzuku na fursa nyingine nyingi zinazotokana na mpango huo wa serikali.