Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Matunda mikataba ya wawekezaji iliyosainiwa na Rais Samia Dubai yawa dhahiri
29 May, 2024
Matunda mikataba ya wawekezaji iliyosainiwa na Rais Samia Dubai yawa dhahiri

#Tayari Kampuni ya Rokosan imewasili kuwekeza kiwanda kikubwa cha mbolea

Imeelezwa kwamba ujio wa mwekezaji wa kampuni ya Rokosan ya nchini Slovakia ni matokeo ya moja kati ya mikataba iliyosainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani alipofanya ziara ya kikazi nchini Dubai wakati wa maonesho ya Dubai –Expo 2020.

Hayo yamebainishwa na Balozi James Bwana aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine kwenye ufunguzi wa warsha iliyoandaliwa na kampuni hiyo kwa lengo la kuitambulisha kampuni na bidhaa itakayokuwa ikizalisha iliyofanyika tarehe 25 Mei, 2022 katika ukumbi wa New Africa Hote Jijini Dar Es Salaam.

Balozi James Bwana alieleza kuwa mazingira rafiki yaliyowekwa na Rais Samia yameendelea kuwavutia wawekezaji wengi wanaoendelea kuonesha nia na kuja kuwekeza nchini, kampuni ya Rokosan ikiwa ni miongoni mwao.
Balozi James Alisema uwepo wa kiwanda cha mbolea kinachotarajiwa kujengwa wilayani Pwani kutaimarisha hali ya kimazingira ya nchi kutokana kiwanda hicho kutumia malighafi za asili zinazopatikana katika mazingira ya kawaida ambapo awali zilikuwa zikitupwa kama uchafu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo akizungumza jambo mbele ya washiriki wawarsha iliyolenga kuitambulisha kampuni ya Rokosan na wabia wake iliyofanyika tarehe 25 Mei, 2022 katika ukumbi wa Four Pointsby Sheraton Jijini Dar Es Salaam

Alisema, kutokana na matumizi hayo ya taka hizo zilizokuwa zikisababisha uchafunzi wa mazingira sasa zitatumika kama malighafi na hivyo kuimarisha uchumi wa wananchi mara baada ya kuuza taka hizo kiwandani lakini pia zitapunguza uchafuzi wa mazingira.

Aliendelea kusema, uwepo wa kiwanda hicho nchini utaongeza usalama wa chakula na kupunguza madhara yaliyotokana na matumizi mabaya ya mbolea zenye kemikali ambazo zimeharibu afya ya udongo kwa kiasi kikubwa.

Aidha, Balozi James alisema, kutokana na aina ya mbolea itakayozalishwa kiwandani hapo kutokuwa na madhara kwa udongo na mazao, mazao yatakayopatikana kufuatia matumizi ya mbolea hiyo yatapata soko la uhakika nje ya nchi na hivyo kuliingizia taifa fedha za kigeni na kuongeza mchango wa Sekta ya kilimo kwenye pato la Taifa.

Balozi James Bwana alihitimisha hotuba yake kwa kuwaalika wawekezaji wengine kufika nchini na kuwekeza katika sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya kilimo, sekta ya Utalii, sekta ya Madini na kwingineko kadri watakavyoona inafaa.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo alisema, moja kati ya majukumu ya Mamlaka ni kuhamasisha uwekezaji wa ndani wa viwanda vya mbolea ili kuwapunguzia wakulima changamoto ya upatikanaji wa mbolea.

Dkt. Ngailo alisema, kufuatia changamoto mbalimbali zikiwemo za ugonjwa wa uvico-19 na vita kati ya Ukraini na Urusi ambayo ni miongoni mwa mataifa yanayozalisha mbolea kwa wingi kumepelekea kuwepo kwa changamoto ya bei na upatikanaji wa mbolea kutokana na ukweli kwamba asilimia 90 ya mbolea inayotumika nchini kuingizwa kutoka nje ya nchi.

Dkt. Ngailo aliwahakikishia ushirikiano wa kutosha wawekezaji hao na kuhakikisha mchakato mzima wa kuanzisha kiwanda hicho cha mbolea ya asili (organic fertilizer) unakamilika na mradi unaanza kwa wakati.

Akizungumzia suala la kiwango cha mbolea kinachohitajika nchini kwa mwaka, Dkt. Ngailo alisema tani laki saba (700000) zinatumika kwa mwaka na kubainisha kuwa kiasi hicho cha matumizi ni kidogo kutokana na wakulima wengi kutokuwa na uwezo wa kununua mbolea kutokana na bei yake kuwa juu.

Aidha, Dkt Ngailo aliwataka wadau pamoja na wawekezaji kuendelea kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa wakulima kwani baadhi yao hawatumii mbolea kutokana na kutokuwa na uelewa wa tija inayotokana na matumizi ya mbolea kwenye kilimo pamoja na wengine kuwa na Imani mgando juu ya matumizi hayo ya mbolea na kueleza matumizi sahihi ya mbolea hayana madhara kwa mlaji.

Washiriki wakifuatilia mada wakati wa warshaya kuitambulisha kampuni hiyo iliyofanyika tarehe 25 Mei, 2022 katika ukumbi wa Four Pointsby Sheraton Jijini Dar Es Salaam. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo

Akizungumzia suala la ubora wa mbolea itakayozalishwa na kiwanda hicho, Dkt. Ngailo aliwahakikisha watanzania na wakulima kwa ujumla kuwa mbolea itakayozalishwa na kiwanda hicho itapimwa ili kujiridhisha na viwango vya ubora vitakavyopatikana kwenye mbolea hiyo kabla ya kuanza kutuka na wakulima kwenye shughuli zao za kilimo.

Kwa upande wa soko, Dkt Ngailo alisema kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha kiasi cha lita milioni ishirini (lita 20000000) kwa mwaka na kubainisha kuwa kiwanda kingine cha Itracom kinachojengwa Jijini Dodoma na kuzalisha tani laki sita za mbolea kwa mwaka soko lake ni la uhakika.

Amesema uhakika wa soko unatokana na malighafi zitakazotumika katika uzalishaji wa mbolea kupatikana nchini kwa wingi na hivyo kuwa na uhakika kuwa bei zitakazouzia bidhaa hizo zitakuwa ni zile ambazo wakulima wanazimudu ikiwa ni pamoja na kuziuzia nchi jirani kiasi cha mbolea kinachobaki baada ya kutosheleza mahitaji ya ndani.

Akizungumzia uzoefu wa kampuni hiyo kwenye biashara ya mbolea Mkurugenzi wa Kampuni ya Rokosan, Adam Zo'ke alisema kampuni yake ina miaka 20 kwenye biashara hiyo na kwamba inatambulika kwenye umoja wa Ulaya na Afrika na kukiri anatarajia kufanya Zaidi biashara ya mbolea barani Afrika.

Alisema mbolea inayozalishwa kiwandani hapo itatokana na vitu vya asili kama vile manyoya ya kuku, kwato, pembe za ng’ombe na wanyama wengine, samadi ya mifugo na nyinginezo jambo litakalosaidia katika kutunza mazingira kwa kiasi kikubwa.

Alisema mbolea hiyo ni rafiki kwa udongo na walaji kutokana na utengenezaji wake kutohusisha kemikali na kwamba ikitumika kwa muda mfupi hurejesha afya ya udongo iliyopotea kutokana na sababu mbalimbali.

Matokeo ya kutumia mbolea itakayozalishwa kiwandani hapo ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hivyo kuwa na uhakika wa chakula, kufungua soko kwa wafugaji kuuza malighafi kwa ajili ya kiwanda hicho, kuboresha bioanuai katika udongo, na ufufuaji wa ardhi ya kilimo iliyoathirika kwa matumizi ya muda mrefu.

Pamoja na hayo Dr. Adam alieleza manufaa mengine kuwa ni kuongeza fursa za ajira ambapo alibainisha kuwa pindi ujenzi utakapoanza watanzania 150 wataajiriwa ili kufanya kazi za ujenzi kiwandani hapo na baada ya ujenzi kukamilika wanatarajia kutoa ajira za kudumu 1000 kwa watanzania na ajira 12 kwa wataalamu kutoka nje ya nchi.