Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Maboresho Mfumo wa mbolea ya ruzuku ni endelevu- waziri Bashe
29 May, 2024
Maboresho Mfumo wa mbolea ya ruzuku ni endelevu- waziri Bashe

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema, hakuna maendeleo yanayotokea kwa msimu mmoja hivyo Wizara ya kilimo inajenga mifumo imara ambayo hata vizazi vijavyo vitaikuta, kuvitumia na kuzalisha kwa tija.


Amesema changamoto ya mfumo wa mbolea ya ruzuku ni kwa sababu ndio unaanza lakini wizara imeiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na watengenezaji wa mfumo kuboresha kadri changamoto zinavyojitokeza.

Waziri Bashe ameyasema hayo leo tarehe 07Januari, 2023 wakati wa kikao baina ya viongozi wa chama na serikali wa Mkoa wa Mbeya, Wakuu na baadhi ya watumishi wa taasisi zilizopo chini ya wizara ya kilimo, wakulima na mawakala wa mbolea kilichofanyika katika ukumbi wa Mkapa jijini Mbeya.

Amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ana utashi wa kisiasa na amekuwa na utayari wa kuwekeza kwenye Sekta ya Kilimo na hivyo kutenga kiasi cha shilingi bilioni mia moja hamsini kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na tumeanza kutoa ruzuku.

Akizungumzia uchache wa vituo vya kuuzia mbolea, Waziri Bashe amewataka Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na maafisa kilimo kuainisha maeneo wanayoweza kuweka vituo vya kuuzia mbolea na kuwasilisha TFRA ili visajiliwe na mawakala wapeleke mbolea karibu na maeneo ya uzalishaji.

"Mbolea haitauzwa kwenye maeneo ambayo hayajasajiliwa kwani kupitia vituo hivyo ndivyo vitakavyosaidia kupanga bei elekezi" waziri Bashe alisisitiza.


Waziri Bashe amewataka wadau mbalimbali wa Sekta ya Kilimo kutambua changamoto, kuzitolea taarifa na kushauri namna nzuri ya kuzitatua na kubainisha kuwa mwelekeo wa wizara ni kutafuta utatuzi wa kudumu wa changamoto hizo.

Ameongeza kuwa, mwaka ujao vituo vya kuuzia mbolea vitaanza biashara hiyo baada ya msimu wa mavuno kuanzia mwezi wa Julai na Agosti ili wakulima waweze kununua pembejeo hizo mapema watunze nyumbani mwao tayari kwa msimu wa kilimo unaofuata.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Stephan Ngailo ameziomba Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya kupitia kamati zao za pembejeo kukaa na kuchagua maeneo wanayopendekeza kupeleka mbolea na kuainisha gharama za usafiri ili kurahisisha katika upangaji wa bei elekezi kwa maeneo hayo.

Kwa upande wa wakulima, Dkt. Ngailo ametoa wito kwa wakulima kuendelea kujisajili ili waweze kunufaika na mbolea za ruzuku aidha, amewatoa hofu kwamba mbolea za ruzuku zitakwisha na kubainisha mbolea ipo ya kutosha na kila mkulima aliyesajiliwa hatakosa mbolea ya ruzuku.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya (W II), Mayeka Simon Mayeka ameishukuru wizara kwa juhudi kubwa za kuwawezesha wakulima kulima kwa tija na kukiri wananchi wamehamasika sana kulima mwaka huu ukilinganisha na msimu uliopita.