Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Itracom yajipanga kutatua kero ya mbolea nchini


Imeelezwa kuwa ifikapo 2030 hakutakuwa na uingizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi kufuatia uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha kiasi kinachotosheleza mahitaji ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 11 Januari, 2023 na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari nchini katika kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Itracom kilichopo Nala Jijini Dodoma.


Dkt. Ngailo amesema ujenzi wa viwanda vya mbolea ni utekelezaji wa sera inayotokana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha ifikapo 2025 uzalishaji wa mbolea nchini unafikia tani 800,000.

Akieleza kuhusu mbolea zilizosajiliwa nchini mpaka sasa, Dkt. Ngailo alisema aina 420 za mbolea zimesajiliwa na zinakidhi viwango vinavyotakiwa nchini.

Aidha, Dkt. Ngailo amesema, Mwekezaji wa kiwanda cha Itracom atazalisha mbolea kulingana na mahitaji ya mlaji baada ya kupima afya ya udongo na kubaini aina ya virutubisho vinavyopungua kwenye shamba lake.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Itracom, Nduwimana Nazaire amesema, awali mwekezaji alijipanga kuzalisha tani laki sita lakini kufuatia mahitaji makubwa ya mbolea nchini atazalisha tani milioni moja kwa mwaka.

Nduwimana amesema, kiwanda hicho kimejikita katika kuzalisha mbolea za asili (organal mineral fertilizer) zinazofanya vizuri kwenye uzalishaji na kimejengwa kwa muda wa mwaka mmoja na miezi mitano mpaka kilipoanza uzalishaji wa awali.