Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
HAKUNA UPUNGUFU WA MBOLEA MBINGA- DC MAKORI
17 Oct, 2025
HAKUNA UPUNGUFU WA MBOLEA MBINGA- DC MAKORI

Mkuu wa wilaya ya mbinga Kisare makori, amesema wamejiridhisha upatikanaji wa mbolea katika wilaya hiyo ni wa uhakika kuelekea msimu mpya wa kilimo wa 2025-26.

Ametoa kauli hiyo baada ya kutembelewa na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Happiness Mbelle akiambatana na watumishi wa Wizara ya Kilimo, Mamlaka na kampuni za mbolea nchini waliofika kueleza sababu ya kuwepo wilayani humo.

Kisare amesema wilaya ya Mbinga inashika nafasi ya Pili kitaifa kwa uzalishaji wa kahawa aina ya arabika, huku akiwaitisha wadau mbalimbali kuwekeza katika zao hilo wilayani mbinga. 

Amesema uzalishaji kwa sasa unaongezeka kila uchao hadi kufikia tani 600 za kahawa, na matarajio ni kuona uzalishaji unaongezeka marambili zaidi ya sasa baada ya kupewa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.

Akieleza sababu za kuwepo wilayani humo, Happiness amesema ni kutekeleza kampeni ya "Mali shambani, silaha mbolea" iliyofanyika katika vijiji vya Utiri na Kigonsera wilayani humo.

Amesema, kampeni hiyo imelenga kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha wakulima kujisajili ili waendelee kunufaika na mbolea za ruzuku zinazotolewa na serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya kuanza msimu wa kilimo 2025/2026.

Akizungumza mara baada ya mafunzo mkulima Ernest Komba amesema kwa mafunzo yaliyotolewa uzalishaji kwa eneo hilo utakuwa mara mbili ya walivyokuwa wakizalisha kwani walikuwa wakitumia pembejeo bila elimu ya kutosha na hivyo kuharibu PH ya udongo na hivyo mbolea kutopelekea matokeo waliyokuwa wakitarajia.