Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Elimu ya matumizi ya mbolea kupunguza kilimo cha kuhamahama Lindi


Mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa mkoa wake kutapunguza kilimo cha kuhamahama kwa wananchi wa Mkoa huo.

Amesema, wananchi wake wamekuwa wakihamahama kutokana na kuamini kwamba pindi shamba likilimwa linapoteza rutuba na hivyo kupelekea wananchi haokuhamia eneo lingine wakiamini kuwa eneo hilo linakuwa na rutuba ya kutosha kustawisha mazao.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 11 Aprili, 2022 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Lindi ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mkulima iliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).

"Kwa hilila uhamasishaji wa matumizi ya mbolea mlilolileta naaamini wananchi wetu watakuwa na makazi ya kudumu. Sasa tuwape uhakika kwamba kwenye ardhi hiyohiyo wakilima kwa kutumia mbolea watavuna mazao ya kutosha". Telack aliongeza.

Maadhimisho hayo ni kilele cha uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa mkoa wa Lindi yaliyoanza mwezi Mei, 2021 kufuatia mkoa huo kuwa na matumizi hafifu ya mbolea ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi kama vile Iringa, Mbeya, Mwanza na maeneo mengine.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akitoa taarifa fupi ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa Mkoa wa Lindi yaliyofanyika katika Kijiji cha Chimbila B wilayani Ruangwa leo tarehe 11 Aprili, 2022.

Akizungumzia sababu zinazopelekea uwepo wa matumizi hafifu ya mbolea kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi, Telack alisema ni kutokuwepo kwa wauzaji wa mbolea katika mikoa ya kusini na kuyataka makampuni yanayojihusisha na biashara ya mbolea kufungua matawi ili kuwawezesha wakulima wa maeneo hayo kupata huduma hiyo.

"Tunahitaji elimu tunahitaji kusaidiwa na ili mtusaidie kwa uharaka leteni tawi karibu, tuwasaidie wakulima naomba tuwasaidie wakulima" Telack alisisitiza.

Kwa upande wa huduma ya upimaji wa afya ya udongo inayoweza kuwasaidia wakulima kujua aina ya udongo na mazao yanayoweza kustawi Telack amelitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI)kufungua tawi katika mkoa huo ili kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Telack aliwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri kuwekeza kwa wakulima na kuhakikisha mazao wanayolima yanawekwa mbolea ili waongeze tija.

Akinukuu kauli ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amesema, Wewe umesema kuona ni kuamini na mimi nasema kuona ni kujifunza na sisi tumejifunza na kuwataka wakulima waliopata elimu hiyo kufikisha elimu hiyo kwa.wakulima wengine ili na wao wapate uelewa huo.

Akihitimisha hotuba yake, Bi. Telack amesema, kwa sababu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza na sisi tuwekeze, naomba sasa tuwekeze kwa wakulima ili mhe. Rais aone tija inayotokana na uwekezaji alioufanya kwenye Sekta ya Kilimo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TFRA, Dkt. Ngailo amesema mamlaka iliamua kufanyauhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea katika mikoa ya Lindi na Mtwara kutokana na maeneo haya kutojihusisha na matumizi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.

Amesema, hiyo ni hatua ya awali katika uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea itakayopelekea wadau na wafanyabiashara wa mbolea kufungua biashara ya mbolea katika mikoa ya Kusini yaani Lindi na Mtwara.

Amesema, kufuatia uwepo wa bandari ya Mtwara itarahisisha usafirishaji wa mbolea kutoka nje ya nchi ya kushishwa moja kwa moja kwenye bandari hiyo na kuwapunguzia wakulima adha ya upatikanaji wa mbolea.

"Tumeona kuanzishwa mashamba darasa ni njia sahihi ya kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea katika kilimo kwani vikundi vya wakulima vilishiriki mwanzo mpaka mwisho katika kuhudumia mashamba darasa hayo" Dkt. Ngailo alisisitiza

Kwa upande wa vikundi vya wakulima kupitia risala yao walieleza manufaa waliyoyapata kufuatia elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na namna walivyohusika katika maandalizi mpaka mavuno ya mazao hayo.

Tanzania Census 2022