Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Dhana potofu kuhusu mbolea yaathiri uzalishaji wa mazao kanda ya Kati


Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Anthony Diallo amesema wakulima wa Kanda ya Kati wanazalisha chini ya kiwango kutokana na dhana potofu ya wakulima kuwa Mbolea inaharibu udongo wa mashamba yao.

Dkt. Diallo amesema hayo wakati akizungumza na Wadau wa Kilimo wa Mkoa wa Singida, ikiwa ni ziara ya Wajumbe wa Bodi na Menejimenti TFRA iliyolenga kutoa Elimu na Kuhamasisha matumizi Sahihi ya Mbolea kwa wakulima.

Amesema wakulima wengi hawataki kutumia Mbolea kwa kudhani kuwa mbolea inaharibu udongo wa mashamba yao na kuamini kuwa itasababisha wavune mazao kidogo jambo ambalo si kweli.

Dkt. Diallo amesema ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na mazao mengi katika eneo dogo ni lazima wahimizwe kutumia Mbolea kwa wakati na kwa usahihi, na kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa Kilimo.

Pamoja na hayo, Dkt. Diallo amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kufuatilia taarifa ya afya ya udogoya maeneo wanayoyasimamia ili wakulima watumie mbolea kulingana na mahitaji ya udongo wanaoulima.

Amesema, taarifa hiyo pia itasaidia wazalishaji kujua aina ya virutubisho vinavyohitajika katika kila eneo la nchi na kuzalisha na kusambaza kiasi cha mbolea kinachotosheleza mahitaji husika.

"Huwezi kutumia Mbolea bila kujua afya ya udongo, hivyo wakulima watumie mbolea kutokana na afya ya udongo wa mashamba yao"
Dkt. Diallo ameongeza

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema Mikoa ya Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa imeendelea kuwa na matumizi madogo ya Mbolea kutokana na mwamko mdogo wa wakulima kutumia Mbolea hali inayosababisha wakulima kuzalisha chini ya kiwango.

Ili kuongeza matumizi ya Mbolea Mkurugenzi Laurent amewataka Maafisa Ugani kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu faida za matumizi ya mbolea ili waweze kutumia mbolea na waweze kuongeza uzalishaji.

Aidha, ameahidi Mamlaka kusimamia zoezi la kufikisha Mbolea kwa wakulima kwa wakati ili kuondoa vikwazo vinavyowafanya wakulima kushindwa kutumia Mbolea kwenye uzalishaji wao.

Kwa upande wa baadhi ya wadau wa kilimo walioshiri katika kikao hicho wameomba mbolea hizo ziwe zinawafikia kwa wakati ili kuwaepushia kadhia wanayoipata pindi msimu wa kilimo unapofika na pembejeo hiyo kukosekana sokoni.