Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Dangote kujenga kiwanda cha mbolea nchini
18 May, 2026
Dangote kujenga kiwanda cha mbolea nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini baada ya Dangote Group kuonesha nia ya kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo uzalishaji wa mbolea kwa ajili ya kukuza sekta ya kilimo nchini.

Hatua hiyo imebainishwa jana tarehe 16 Mei 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam katika mazungumzo kati ya Rais Dkt. Samia na Mwenyekiti pamoja na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaji Aliko Dangote, ambapo pande hizo mbili zilijadili fursa za uwekezaji na ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Katika mazungumzo hayo, Alhaji Dangote ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, akieleza kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutatua changamoto za wawekezaji zimeongeza ufanisi wa shughuli za uzalishaji na kuimarisha imani ya wawekezaji nchini.

Aidha, Dangote amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa pembejeo za kilimo na bidhaa za viwandani katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji, upatikanaji wa rasilimali pamoja na soko la uhakika.

Kwa upande wake, Rais Dkt. Samia amemkaribisha Alhaji Dangote kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa mbolea nchini akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea ukuaji wa sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa ajili ya chakula na biashara.

Mbali na tasnia ya mbolea, mazungumzo hayo pia yalihusu maeneo mengine ya uwekezaji ikiwemo nishati, gesi, viwanda na miundombinu, hatua inayotarajiwa kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Ushirikiano huo unaendelea kufungua ukurasa mpya wa uwekezaji nchini huku tasnia ya mbolea ikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayosaidia kuongeza tija ya kilimo na kuimarisha usalama wa chakula nchini.