Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Waziri wa Kilimo atoa rai halmashauri kuwekeza katika viwanda vya mbolea hai
30 Apr, 2026
Waziri wa Kilimo atoa rai halmashauri kuwekeza katika viwanda vya mbolea hai

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amezitaka halmashauri nchini kutumia taka ozo kama fursa ya kiuchumi kwa kuanzisha viwanda vya kuzalisha mbolea hai, hatua ambayo itasaidia kuongeza upatikanaji wa mbolea, kuimarisha uzalishaji wa kilimo na kuhifadhi mazingira.

Mhe. Chongolo ametoa rai hiyo leo Aprili 28, 2026, wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma.

Amezipongeza Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Moshi kwa hatua walizochukua za kuanzisha viwanda vinavyozalisha mbolea hai kwa kutumia taka ozo, akieleza juhudi hizo zimeonesha namna taka zinavyoweza kubadilishwa kuwa rasilimali yenye manufaa kwa sekta ya kilimo na mazingira.

Aidha, amezitaka halmashauri nyingine kuiga mfano huo kwa kutumia taka zinazozalishwa kwa wingi katika maeneo yao kuanzisha miradi ya uzalishaji wa mbolea hai, hatua itakayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira sambamba na kuongeza upatikanaji wa pembejeo muhimu kwa wakulima.

Akitoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Chongolo amesema taka zinazokusanywa katika dampo la Pugu zinaweza kutumika kuzalisha mbolea hai kwa kiwango kikubwa, jambo litakalosaidia kupunguza mrundikano wa taka, kuboresha usafi wa mazingira na kuchangia maendeleo ya kilimo chenye tija nchini.