Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

Announcements

TAARIFA KWA UMMA: BEI ELEKEZI KWA MBOLEA ZA KUPANDIA NA KUKUZIA KWA MSIMU WA KILIMO 2023/2024 (Toleo la 23)


TAARIFA KWA UMMA: BEI ELEKEZI KWA MBOLEA ZA KUPANDIA NA KUKUZIA KWA MSIMU WA KILIMO 2023/2024 (Toleo la 23)

  • 1.0UTANGULIZI

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Authority - TFRA) kwa niaba ya Wizara ya Kilimo ina jukumu la kutoa bei elekezi ya mbolea ambapo mbolea zinatakiwa kuuzwa kwa bei elekezi au chini yake. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.

Katika kutekeleza jukumu lake la kisheria, TFRA imefanya mapitio ya bei elekezi kwa mbolea aina kumi na nne (14); saba (7) zinazoingizwa kutoka nje (DAP, UREA, CAN, SA, NPKs, YARA Cereal, YARA Otesha) na saba (7) zinazozalishwa na viwanda vya mbolea vya Itracom (Fomi Otesha, Fomi Kuzia, Fomi Nenepesha) na Minjingu (Nafaka Plus, Top Dressing, Pamba, Tobacco, Chai, Coffee).

Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia tarehe 01 Septemba, 2023 Bei zinapatikana kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA); Bei Elekezi za mbolea Septemba 2023 na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara). Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa mbolea inauzwa nchini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia tasnia ya mbolea.

  • 2.0MJENGEKO WA BEI ELEKEZI

Kwa kuwa mbolea za DAP, UREA, CAN, SA, NPK YARA Cereal na YARA Otesha ni mbolea zinazoingizwa kutoka nje ya nchi; bei elekezi imezingatia gharama za manunuzi, usafirishaji, uingizaji, ufungashaji, usambazaji pamoja na faida atakayopata mfanyabiashara. Aidha, kwa mbolea zinazozalishwa nchini (Fomi Otesha, Fomi Kuzia, Nafaka Plus, Top Dressing, Minjingu Pamba, Minjingu Chai na Minjingu Coffee ) bei elekezi imezingatia gharama za upatikanaji wa malighafi, uzalishaji, vifungashio, kufungasha, usimamizi na faida ya mzalishaji na muuzaji wa rejareja hadi kumfikia mkulima kwa lengo la kumpunguzia makali ya bei.

  • 3.0BEI ZA MBOLEA YA RUZUKU KWA WAKULIMA

Serikali imeelekeza aina moja ya mbolea kuuzwa kwa bei tofauti kwa wakulima nchini kutokana na umbali wa kituo cha mauzo. Aidha, hakuna mfanyabiashara atakeyeruhusiwa kuuza mbolea nje ya mpango wa ruzuku. Hivyo, tofauti kati ya bei elekezi kwa kila eneo na bei ya mkulima italipwa na Serikali kama ruzuku kwa mkulima kama jedwali linavyoonyesha hapo chini.

BEI ZA MBOLEA ZINAZOINGIZWA KUTOKA NJE YA NCHI

AINA YA MBOLEA

BEI YA CHINI (SHILINGI)

BEI YA JUU (SHILINGI)

DAP

67,625

80,000

UREA

58,568

70,000

CAN

48,671

65,000

SA

39,152

50,000

NPKs

67,935

80,000

YARA OTESHA

67,516

80,000

YARA CEREAL

62,935

75,000

BEI ZA MBOLEA ZINAZOZALISHWA NDANI YA NCHI

AINA YA MBOLEA

BEI YA CHINI (SHILINGI)

BEI YA JUU (SHILINGI)

FOMI OTESHA

68,378

75,000

FOMI KUZIA

68,196

75,000

NAFAKA PLUS

66,229

75,000

TOP DRESSING

66,229

75,000

MINJINGU PAMBA

71,229

80,000

MINJINGU CHAI

71,229

80,000

MINJINGU COFFEE

71,229

80,000

  • 4.0USIMAMIZI WA BEI ELEKEZI

Kwa kuwa mbolea zote zinauzwa katika mpango wa ruzuku, Serikali kupitia TFRA imesajili waingizaji na wazalishaji wa mbolea pamoja na mawakala wanaosambaza na kuuza mbolea kwa wakulima na kuwapa namba maalum za utambulisho. Hata hivyo, ili azma ya Serikali itimie ni muhimu kwa Mamlaka zote husika katika ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika namba ya uwakala na bei elekezi sehemu zinazoonekana kwa urahisi kwa wanunuzi. Pia, ni vema Mamlaka hizo zikasimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa ruzuku ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu uzingatiaji wa bei za mbolea ya ruzuku na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima katika maeneo husika. Aidha, endapo bei hizi hazitaakisi uhalisia wa kijiografia na miundombinu ya eneo husika, nitoe rai kwa Kamati za Pembejeo za Mikoa na Wilaya kupitia na kufanya maboresho kadiri watakavyoona inafaa.

  • 5.0UDHIBITI WA UTOROSHWAJI WA MBOLEA NJE YA NCHI

Pamoja na kwamba mpango wa ruzuku ya mbolea unalenga kuwapunguzia makali ya bei wakulima; wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wanaweza kutumia fursa hiyo kuwalaghai wakulima na kununua mbolea kwa majina yao na baada ya hapo kuitorosha mbolea hiyo kwenda nchi jirani. Hali hii itahatarisha utoshelevu wa mbolea kwa wakulima wetu na pia kuingizia hasara Serikali katika fedha inazotoa kama ruzuku kwa lengo la kumnufaisha mkulima na kuongeza uzalishaji nchini. Pamoja na uelimishaji ambao Serikali inaendelea kuufanya ni vyema Mamlaka zote za Serikali zikashirikiana na wadau wote hususan katika mikoa ya mipakani kama Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Kilimanjaro, Arusha na mikoa mingine kuhakikisha mbolea ya ruzuku haitoroshwi kwenda nchi jirani.

Vilevile, natoa onyo kwa wafanyabiashara wachache wenye tabia hizo au mpango wa kutorosha mbolea ya ruzuku kwenda nchi jirani kutothubutu kufanya hivyo kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi itakapothibitika. Aidha, endapo kutakuwa na haja ya wafanyabiashara kuuza mbolea nje ya nchi, basi wafanye hivyo kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi na sio kutorosha mbolea ya ruzuku.

  • 6.0HITIMISHO

Ni matumaini ya Serikali kuwa, mpango wa ruzuku ya mbolea utawezesha wakulima kutumia mbolea zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji na tija kwa ajili ya utoshelevu wa chakula na kuzalisha malighafi ili kuimarisha uchumi wa viwanda. Hivyo, niwakumbushe wataalamu na wadau wa kilimo kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo. Aidha, natoa wito kwa Mamlaka zote katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika usimamizi wa mbolea ya ruzuku ili Serikali ifikie azma yake na pia mkulima aweze kutumia fursa hii kubadilisha maisha yake kupitia kilimo.

Bei elekezi mpya za mbolea Septemba 2023

Dkt. Stephan E. Ngailo

MKURUGENZI MTENDAJI

Septemba 01, 2023