Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

Announcements

TAARIFA KWA UMMA:BEI ELEKEZI KWA MBOLEA ZA KUPANDIA NA KUKUZIA KWA MSIMU WA KILIMO 2022/2023


1.0UTANGULIZI

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Authority - TFRA) kwa niaba ya Wizara ya Kilimo ina jukumu la kutoa bei elekezi ya mbolea kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini ambapo mbolea zinatakiwa kuuzwa kwa bei elekezi au chini yake. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.

Katika kutekeleza jukumu lake la kisheria, TFRA imefanya mapitio ya bei elekezi kwa mbolea aina tatu zinazozalishwa na kiwanda cha mbolea cha Itracom kinachozalisha mbolea za kupandi na kukuzia (Fomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha) katika kila kituo cha mauzo ambazo zitaanza kutumika tarehe 20 Disemba, 2022 (Bei zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Kilimo; www.kilimo.go.tz, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA); www.tfra.go.tz na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara). Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa mbolea inauzwa nchini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia tasnia ya mbolea.

  • 2.0MJENGEKO WA BEI ELEKEZI

Kwa kuwa mbolea za Kampuni ya ITRACOM Fertilizer Ltd zinazalishwa hapa nchini, bei elekezi imezingatia gharama za upatikanaji wa malighafi, uzalishaji, vifungashio, kufungasha usimamizi na faida ya mzalishaji na muuzaji wa rejareja kusambaza hadi kumfikia mkulima.

  • 3.0BEI ZA MBOLEA YA RUZUKU KWA WAKULIMA

Serikali imeelekeza aina moja ya mbolea kuuzwa kwa bei inayofanana kwa wakulima nchini kote (pan territorial pricing). Hivyo, kutokana na kuwa mzalishaji amefungasha mbolea kwenye mifuko yenye uzito wa kilo 25; bei elekezi ya mkulima kwa mbolea aina yaFomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha itakuwa Shilingi 35,000 baada ya kuweka ruzuku ya Serikali. Aidha,hakuna mfanyabiashara atakeye ruhusiwa kuuza mbolea nje ya mpango wa ruzuku. Hivyo, tofauti kati ya bei elekezi kwa kila eneo na bei ya mkulima italipwa na Serikali kama ruzuku kwa mkulima kwa lengo la kumpunguzia makali ya bei.

  • 4.0USIMAMIZI WA BEI ELEKEZI

Kwa kuwa mbolea zote zinauzwa katika mpango wa ruzuku, Serikali kupitia TFRA imesajili waingizaji na wazalishaji wa mbolea pamoja na mawakala wanaosambaza na kuuza mbolea kwa wakulima na kuwapa namba maalum za utambulisho. Hata hivyo, ili azma ya Serikali itimie ni muhimu kwa Mamlaka zote husika katika ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika namba ya uwakala na bei elekezi sehemu zinazoonekana kwa urahisi kwa wanunuzi. Pia ni vema mamlaka hizo zikasimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa ruzuku ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu uzingatiaji wa bei za mbolea ya ruzuku na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima katika maeneo husika.

  • 5.0UDHIBITI WA UTOROSHWAJI WA MBOLEA NJE YA NCHI

Pamoja na kwamba mpango wa ruzuku ya mbolea ni neema kwa wakulima, wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wanaweza kutumia fursa hiyo kuwalaghai wakulima na kununua mbolea kwa majina yao na baada ya hapo kutorosha mbolea kwenda nchi jirani. Hali hii itahatarisha utoshelevu wa mbolea kwa wakulima wetu na pia kuingizia hasara Serikali katika fedha inazotoa kama ruzuku kwa lengo la kumnufaisha mkulima na kuongeza uzalishaji nchini. Pamoja na uelimishaji ambao Serikali inaendelea kuufanya ni vyema Mamlaka zote za Serikali zikashirikiana na wadau wote hususan katika mikoa ya mipakani kama Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Kilimanjaro, Arusha na mikoa mingine kuhakikisha mbolea ya ruzuku haitoroshwi kwenda nchi jirani.

Vilevile, Mamlaka inatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wachache wenye tabia hizo au mpango wa kutorosha mbolea ya ruzuku kwenda nchi jirani kutothubutu kufanya hivyo kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao pindi itakapothibitika. Aidha, endapo kutakuwa na haja ya wafanyabiashara kuuza mbolea nje ya nchi, basi wafanye hivyo kwa kuzingatia sheria za nchi na sio kutorosha mbolea ya ruzuku.

  • 6.0HITIMISHO

Ni matumaini ya Serikali kuwa, mpango wa ruzuku ya mbolea utawezesha wakulima kutumia mbolea zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji na tija kwa ajili ya utoshelevu wa chakula na kuzalisha malighafi ili kuimarisha uchumi wa viwanda. Hivyo, niwakumbushe wataalam na wadau wa kilimo kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo. Aidha, natoa wito kwa Mamlaka zote katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika usimamizi wa mbolea ya ruzuku ili Serikali ifikie azma yake na pia mkulima aweze kutumia fursa hii kubadilisha maisha yake kupitia kilimo.

20221220 market prices for fomi otesha fertilizers (itracom tz ltd)

20221220 market prices for fomi kuzia fertilizers (itracom tz ltd)

20221220 market prices for fomi nenepesha fertilizers (itracom tz ltd)

Dkt. Stephan E. Ngailo

MKURUGENZI MTENDAJI

Desemba 20, 2022