TAARIFA KWA UMMA
1.0 UTANGULIZI
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Authority - TFRA) ina jukumu la kutoa bei elekezi kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za Mwaka 2011 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.
Katika kutekeleza jukumu lake la kisheria, TFRA imefanya mapitio ya bei elekezi kwa aina kumi na saba (17) za mbolea ambapo aina nane (8) ni mbolea zinazoingizwa kutoka nje (DAP, UREA, CAN, SA, NPKs, MoP, NPK Tobacco na TSP) na aina tisa (9) ni mbolea zinazozalishwa ndani ya nchi na Kampuni ya Itracom (Fomi Otesha, Fomi Kuzia na Fomi Nenepesha) na Kampuni ya Minjingu (Minjingu Nafaka Plus, Minjingu Top Dressing, Minjingu Pamba, Minjingu Chai, Minjingu Coffee, na Minjingu Tobacco).
Bei elekezi zitaanza kutumika kuanzia tarehe 21 Agosti, 2024 (Bei zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Kilimo; www.kilimo.go.tz, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA); www.tfra.go.tz na Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara). Lengo la kufanya mapitio na kutangaza bei elekezi ni kuhakikisha kuwa mbolea inauzwa kwa bei inayoendana na gharama halisi za soko. Wafanyabiashara wa mbolea wanatakiwa kuuza mbolea hizo kwa bei elekezi au chini yake.
2.0 MJENGEKO WA BEI ELEKEZI
Kwa mbolea zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, bei elekezi zimezingatia gharama za manunuzi kutoka kwenye chanzo, usafirishaji na bima hadi kuifikisha nchini, gharama ya kubadilisha fedha, uondoshaji wa shenena bandarini, tozo za Mamlaka za Serikali, ufungashaji, usambazaji ndani ya nchi pamoja na faida za wafanyabiashara. Aidha kwa mbolea zinazozalishwa ndani ya nchi, bei elekezi zimezingatia gharama za uzalishaji zikijumuisha upatikanaji wa malighafi, uendeshaji, usimamizi, usambazaji wa mbolea na faida za wazalishaji na wafanyabiashara.
3.0 BEI ZA MBOLEA YA RUZUKU KWA WAKULIMA
Katika msimu wa 2024/25 mbolea itaendelea kuuzwa kwa wakulima kwa bei ya ruzuku kulingana na umbali kutoka kwenye chanzo. Aidha, hakuna mfanyabiashara atakeye ruhusiwa kuuza mbolea nje ya Mpango wa Ruzuku isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka TFRA. Aidha, tofauti ya bei halisi ya soko na bei elekezi ya mkulima kwa kila eneo italipwa na Serikali kama ruzuku kwa wakulima kwa lengo la kuwapunguzia makali ya bei.
4.0 USIMAMIZI WA BEI ELEKEZI
Kwa kuwa mbolea zote zinauzwa katika Mpango wa Ruzuku, Serikali kupitia TFRA imesajili Waingizaji na Wazalishaji wa mbolea pamoja na Mawakala wanaosambaza na kuuza mbolea kwa wakulima kwa kuwapa namba maalum za utambulisho. Hata hivyo, ili azma ya Serikali itimie ni muhimu kwa Mamlaka zote husika katika ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika namba ya uwakala na bei elekezi sehemu zinazoonekana kwa urahisi kwa wanunuzi. Pia ni vema Mamlaka hizo zikasimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu uzingatiaji wa bei elekezi za mbolea na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima katika maeneo husika.
5.0 HITIMISHO
Ni matumaini ya Serikali kuwa, Mpango wa Ruzuku ya Mbolea utawezesha wakulima kutumia mbolea zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji na tija ili kuimarisha usalama wa chakula, upatikanaji wa malighafi za viwanda na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Hivyo, niwakumbushe wataalam na wadau wa kilimo kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo. Aidha, natoa wito kwa Mamlaka zote katika ngazi za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika usimamizi wa mbolea za ruzuku ili Serikali ifikie azma yake na pia mkulima aweze kutumia fursa hii kuongeza tija katika uzalishaji na kuboresha maisha yao kupitia kilimo.
IMETOLEWA NA MAMLAKA YA UDHIBITI WA MBOLEA TANZANIA
Agosti 21, 2024