Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Waziri Bashe azitaka kampuni za mbolea kusajiliwa


Mfumo usajili wa wakulima wazinduliwa

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuwasilisha majina ya kampuni zitakazokiuka takwa la kusajiliwa ili kushiriki kwenye zoezi la usambaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima nchini.

Alisema yuko tayari kuzifutia leseni za usajili kampuni zote zitakazokiuka takwa la kujisajili wao na wakala wao.

Waziri Bashe alisema hayo jana tarehe 4 Julai, 2022 wakati wa Uzinduzi wa Mfumo wa kidijitali wa Usajili wa Wakulima na Mwongozo wa Utoaji wa mbolea ya Ruzuku kwa msimu wa kilimo 2022/2023 uliofanyika katika ukumbi wa kijiji Chamwino Jijini Dodoma.

Alisema makampuni yote yatakayohusika na kuingiza wa mbolea za ruzuku lazima yafuate taratibu za serikali ili kuepuka udanganyifu.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kushoto) na Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde wakiwa wamenyanyua mfuko wa ruzuku ya mbolea ikiwa ni mfano wa mifuko itakayotumika wakati wa utoaji wa mbolea za ruzuku Chamwino jijini Dodoma


"Sitakuwa tayari kuziangalia kampuni zitakazofanya udanganyifu, nahitaji kuona kila kampuni inafuata utaratibu uliowekwa na Serikali wa uingizaji wa mbolea nchini," alisema Bashe.

Pamoja na hayo, Waziri Bashe alionya mfanyabiashara yeyote anayejiandaa kuingia kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku akidhani itakuwa kama ilivyokuwa wakati wa vocha imekula kwake.

"Yeyote anayejiandaa kuingia kwenye mfumo wa ruzuku za vocha imekula kwake". Bashe alisisitiza

Akizungumzia kuhusu vipaumbele vya utoaji ruzuku ya mbolea Bashe alisema serikali itatoa kipaumbele kwa viwanda vya ndani ili kuchochea uwekezaji katika tasnia hiyo nchini.

Katika hatua nyingine Bashe ameiomba TAMISEMI kuondoa adhabu ya kulima kwa wanafunzi waliofanya makosa kama adhabu kwani kufanya hivyo kunawafanya watoto kukichukia kilimo kutoka wakiwa wadogo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Andrew Masawe alisema utoaji wa mbolea ya ruzuku ni moja kati ya mikakati ya kufanikisha agenda 10/30 inayohitaji kuona mchango wa sekta ya kilimo unakua kwa asilimia 10 ifikapo 2030.


Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde aliwaagiza wakuu wa Mikoa na Wilaya kufuatilia kwa kina Maafisa Kilimo kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijiji na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kitalaamu badala ya kufanya kazi tofauti na utaalam wao.

Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa wanafanya hivyo, kwa sababu wanajua maafisa kilimo wengi wanafanya kazi tofauti na taaluma yao ambayo imewaweka kazini.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo aliishkuru wizara ya kilimo kwa ushirikiano na maelekezo inayoyatoa katika kuhakikisha mkakati wa usambaji mbolea ya ruzuku unafanikiwa.


Alisema katika kuhakikisha suala la utoaji ruzuku linafanikiwa TFRA ikishirikiana na CRDB bank na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom wameandaa mfumo wa kidigitali wa usajili, wameandaa mwongozo pamoja na fomu kwa ajili ya usajili wa wakulima.


Alisema wao kama TFRA wako tayari kutekeleza maagizo waliopewa na wizara na kuhakikisha wakulima ndio wanaonufaika na mbolea hizo.

Tanzania Census 2022