Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Wakulima nchini waanza kunufaika na mbolea ya ruzuku


Wananchi wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Tabora tayari wameanza kunufaika na mbolea ya ruzuku ambapo mpango wa utoaji wa mbolea hiyo kwa wakulima ulizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima yaani nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya Mwakangale Jijini Mbeya.

Akizindua mfumo huo, Rais Samia aliagiza kuwa wakulima waanze kunufaika na mbolea ya ruzuku ifikapo Agosti 15, 2022 ili kuwawezesha wakulima kuwa na mboleawakielekea msimu wa kilimo kwa ajili ya maandalizi.

Taarifa ya kuanza rasmi kwa mauziano ya mbolea hiyo ya ruzuku yametolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Stephan Ngailo jana tarehe 21 Agosti, 2022 Jijini dar es Salaam na kubainisha kuwa mpaka siku hiyo wakulima wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Tabora wameanza kuununua mbolea kwa bei elekezi ya ruzuku.

Ameongeza maeneo mengine yatakayoanza kuuza mbolea ya ruzuku kuanzia tarehe 22 Agosti, 2022 ni Songea, Mbinga Lindi na Mtwara huku akitoa wito kwa wakulima kujitokeza kwa wakati kujisajili ili kunufaika na mbolea hizo huku akisisitiza hakuna mkulima atauziwa mbolea hizo pasipo kusajiliwa.

Akizungumza wakati akinunua mbolea hizo kwa wakala wa kampuni ya ETG Mkoani Tabora, Mkulima Salum Mchele alikiri kuwa kilimo cha nyanya na matikiti kinatumia mbolea nyingi na kueleza kuwa msimu uliopita wa kilimo walinunua mbolea kwa bei kuanzia shilingi 140,000 hadi shilingi 160,000 na kuonesha furaha yake kwamba sasa wauzaji wanatekeleza agizo la Rais Samia kwa kuuza mbolea kwa bei elekezi ya shilingi elfu 70.

Pamoja na hatua hiyo ya serikali kwa kushirikiana na waingizaji na wauzaji wa mbolea kuanza kuuzaji mbolea za ruzuku kwa wakulima Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Kanda ya Kati, amewataka wakulima kununua mbolea kwa namba za utambulisho walizopewa wakati wa usajili na si kutoa namba kwa mtu mwingine ili aitumie kununua mbolea badala yako.

Alisema kufanya hivyo hakutafanikisha zoezi la kununua mbolea kwani namba pekee haimfanyi mkulima kununua mbolea na kuelezavipo vigezo tofautitofauti vinavyoangalia kulingana na taarifa zilizopo kwenye mfumo wa uuzaji wa mbolea hizo za ruzuku.

Kuanza kwa uuzaji huo wa mbolea kumefuata mara baada ya kutolewa kwa mafunzo ya mfumo wa biashara ya mbolea ya ruzuku kwa mawakala kupitia mfumo wa kidijitali wa ruzuku ya mbolea kwa msimu wa kilimo 2022/2023.