Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Wafanyabiashara wa mbolea waondolewa hofu mizigo kucheleweshwa bandarini


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akiambatana na wafanyabiashara wa mbolea nchini wamekutana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eric Hamissi kujadili namna bora ya kutatua changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara hao nchini.

Kikao hicho kilifanyika jana tarehe 18 Machi, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa bandari Jijini Dar es Salaam na kufikia mwisho mzuri baada ya wafanyabiashara kuondolewa wasiwasi wa mizigo yao kuchelewa kupakuliwa katika bandari hiyo kufuatia juhudi shirikishi baina ya TFRA, TPA na wafanyabiashara wa mbolea.

Mkurugenzi wa bandari Eric Hamissi na wataalam wake wakiwa katika kikao cha utendaji baina yao, TFRA na wafanya biashara wa mbolea

Akiwasilisha changamoto za wafanyabiashara hao, Dkt. Ngailo alisema ni pamoja na ucheleweshwaji wa kushusha shehena ya mbolea mara inapowasili bandarini, uhaba wa vifaa kwa ajili ya upakuaji wa shehena za mbolea, ongezeko la gharama zinazolipwa kwa wamiliki wa meli kutokana na meli zenye shehena ya mbolea kuchukua muda mrefu kutia nanga na kushusha mzigo.

Aidha, Dkt. Ngailo alisema changamoto hizo zinapelekea kupanda kwa gharama ya mbolea pindi zinapowafikia wakulima kutokana gharama kuingizwa kwenye bei ya mbolea inayowaathiri wakulima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Erick Hamissi, alisema zipo changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa mizigo kwa wakati ikiwa ni pamoja na uwepo wa mvua kwa mwezi Januari uliopelekea baadhi ya mizigo kutoshushwa kwa kuwa wakati wa mvua zoezi la kushusha aina fulani ya bidhaa husitishwa pamoja na wafanyabiashara wenyewe kuleta malori machache ya kubeba mzigo wakati wanapakua mzigo mkubwa .

Pamoja na hayo, Mkurugenzi Hamissi aliwataka wafanyabiashara hao kuimarisha mawasiliano baina yao na bandari kwa kutoa taarifa ya mizigo inayotarajiwa kufika kwa wakati ili utaratibu wa kushusha mizigo hiyo iwekwe ili kupunguza uchelewevu.

Aidha, Hamissi amesema, TPA ipo katika harakati za kuandaa Vigezo muhimu vya ufanyaji kazi (Key Performance Indicator (KPI) kwa watumishi wa bandari na wadau wake na kuiomba TFRA kusaidia pindi itakapokamilika kuwafikishia wafanyabiashara wa mbolea vigezo hivyo ili kusaidia katika kupima utendaji kazi wa pande zote.

Alisema, KPI zitasaidia katika kuongeza ufanisi katika utendaji na kupunguza malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wadau wa bandari nchini.

Alisema, kwa upande wao wanajitahidi na wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa ueledi ili kufikia matarajio ya wateja wao.

Kikao hicho ni utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kwa Mkurugenzi wa TFRA mara baada ya kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wafanyabiashara wa mbolea alipokutana nao Jijini Dodoma hivi karibuni.

Tanzania Census 2022