Udhibiti wa mbolea unalenga kuleta ushindani - Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA Dkt Diallo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) amesema lengo la selikari la kudhibiti pembejeo muhimu ya mbolea nchini ni kuhakikisha kuwa inazalishwa kwa ubora unaotakiwa na hivyo kuleta ushindani katika soko.
Dkt Diallo ametoa tafsiri hiyo leo tarehe 15 Machi, 2023 alipofanya ziara iliyolenga kujifunza utendaji kazi kiwandani hapo na kufanya mazungumzo na uongozi wa juu wa kiwanda hicho.
Akitoa tafsiri ya neno udhibiti wakati akifafanua jukumu mojawapo la TFRA, Dkt. Diallo alisema mosi ni kuruhusu ushindani ili kupata mbolea bora na huduma bora kwa wakulima.
Amesema, TFRA ipo mlangoni kumruhusu mwekezaji katika tasnia ya mbolea anayeona kuwa ameshindwa kuzalisha aache na kuwasaidia wenye nia ya kufanya hivyo kuendelea kuzalisha hivyo kuwawezesha wakulima kupata huduma ya mbolea.
"Tupo mlangoni kumfungulia anayetaka kutoka atoke akishindwa na anayetaka kuingia aingie" Dkt. Diallo aliongeza.
"Jukumu letu pia sio upolisi, sisi sio polisi ndio maana tunakuwa na sheria inayoruhusu kutoa adhabu kwa mwekezaji/ mfanyabiashara anayekiuka kanuni, taratibu na sheria inayosimamia tasnia ya mbolea, ukitekeleza masharti unaendelea na kazi ukishindwa una adhibiwa" Dkt. Diallo alisisitiza
Kufuatia maelezo hayo, Dkt. Diallo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuheshimu na kuzingatia matakwa ya sheria, miongozo na taratibu kama zinavyojieleza.
"Tunawategemea sana na wakulima wanawategemea sana, tunadhani kwamba hamtaweza kutuangusha na ushirikiano utakuwa mkubwa tunapoingia kuanza kazi kwa pamoja". Dkt. Diallo alimaliza kuzungumza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Tosky Hans ameeleza kuwa kiwanda hicho kimekuwa na mahusiano ya karibu na TFRA tangu kuanzishwa kwa Mamlaka miaka 10 iliyopita.
Amesema kiwanda hicho kinazalisha mbolea kwa ajili ya mazao mbalimbali kina uzoefu wa miaka 20 tangu kuanzishwa kwake na kimepitia changamoto nyingi lakini ni sehemu ya mafunzo na kuboresha shughuli zao.
"Imekuwa ni safari ndefu mpaka kufika hapa. Tulipo sasa tuna uhakika kwamba mkulima anapata mbolea bora inayokidhi mahitaji" Hans alisisitiza.
Hans ameongeza kuwa, awali wakulima walizoea kutumia mbolea kwa mazoea na hivyo kutoleta tija inayokusudiwa. Aliendelea kueleza kutokana na hali hiyo kiwanda hicho kimeamua kufanya tafiti kwa kanda zote nchini ili kujua mahitaji ya mbolea kwa kila kanda kulingana na virutubisho vinavyokosekana kwenye udongo wa eneo husika.