Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA yawajengea uwezo vijana wanufaika wa BBT kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea
21 Sep, 2024
TFRA yawajengea uwezo vijana wanufaika wa BBT kushiriki  kikamilifu  kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo kupitia Vyuo vya Mafunzo vya Wizara ya Kilimo (Ministry of Agriculture Training Institutes - MATIs) imewajengea uwezo Vijana 170 wa Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow - BBT) katika masuala mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza leo tarehe 21 hadi tarehe 22 Septemba, 2024 kwenye kituo cha BBT Chinangali II Jijini Dodoma ambapo vijana hao wamepata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na uanzishwaji na uendeshaji wa biashara ya mbolea kwa mujibu wa Sheria ya Mbolea Na. 9 ya mwaka 2009.

Akifungua mafunzo hayo Dkt. Mashaka Mdangi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka Wizara ya Kilimo  amesema kuwa kilimo ni muhimu kwa mahitaji ya binadamu na viumbe hai kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Mdangi amezitaka taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kutumia uwezo wao wote kuhakikisha  kilimo kinakua ili kiweze kuchangia katika usalama wa chakula na lishe nchini, kuinua pato la mkulima ili kupunguza umasikini, kuongeza ajira na hatimaye ziada kuuzwa nje na kuwalisha wengine kibiashara kama dira ya Wizara ya Kilimo inavyofafanua.

“Ili tuweze kukuza kilimo hatuna budi kuhakikisha mimea inapata virutubisho na madini stahiki, vitu hivyo vinapatikana kutoka kwenye mbolea.

Wataalamu watatoa somo hapa na kila mmoja atamaliza mafunzo akiwa ameiva vizuri” Dkt. Mdangi alisisitiza.

Ameeleza kuwa, fursa iliyotolewa kwa vijana wa BBT na TFRA itakuwa mkombozi kwani mafunzo yanayotolewa yatawasaidia wao pamoja na wakulima wengine watakaosikia shuhuda za kilimo cha kisasa kutoka kwa washiriki wa mafunzo.

“Nimeambiwa kuwa mafunzo haya yanalenga kuwaonesha fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mbolea ambazo ni pamoja na kufanya biashara ya mbolea na kuwa miongoni mwa wauzaji wa mbolea yaani Mawakala wa mbolea".

Dkt. Mdangi amesisitiza kuwa, Wizara ya Kilimo inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara ya mbolea ikiwa ni pamoja na uwepo wa takribani ghala 987 zenye uwezo wa kuhifadhi mbolea tani 458,610 nchini.

Mwisho Dkt. Mdangi amesistiza TFRA na taasisi nyingine chini ya Wizara ya Kilimo kuendeleza utaratibu wa kufanya mafunzo kama haya kupitia Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vilivyopo nchini. TFRA imeshauriwa pia kuendelea kuandaa mafunzo kama hayo kwa vijana wengi wanaojihusisha na kilimo ili kutoa uelewa wa masuala ya mbolea.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa TFRA Kanda ya Kati, Allan Marik amesema, mafunzo yanayotolewa yanajitosheleza katika kumwezesha mshiriki kujihusisha na biashara ya mbolea na kueleza baada ya mafunzo washiriki wote watatunukiwa vyeti vya mafunzo hayo.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye miradi ya kimkakati ili kufikia Agenda 10/30; Kilimo ni Biashara yenye lengo la kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakua kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030.

Mafunzo yanatarajiwa kufungwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent atakayewatunuku vyeti washiriki 170 wa mafunzo hayo.

Mbolea Day