TFRA yaridhishwa na hali ya upatikanaji mbolea Njombe

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo amekagua na kujiridhisha na hali ya upatikanaji wa mbolea katika Mkoa wa Njombe.
Amefanya ukaguzi huo leo tarehe 20 Julai, 2023 katika ghala la kampuni la mbolea la OCP lililopo Makambako Mkoa wa Njombe na kubaini uwepo wa tani 15,477 za mbolea.
Baada ya ukaguzi huo, Dkt. Ngailo ameeleza kuwa kiasi cha mbolea kilichopo kitatosheleza mahitaji ya mbolea kwa wakulima wa Mkoa huo wanaojikita kwenye kilimo katika maeneo ambayo mvua zinawahi kuanza huku akitolea mfano Wilaya ya Makete.
Katika ukaguzi huo, Dkt. Ngailo ameambatana na Meneja wa TFRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Michael Sanga.
Aidha, Dkt. Ngailo ameuelekeza uongozi wa kampuni hilo kufungua vituo katika maeneo ya vijijini pamoja na kutoa mbolea kwa mawakala walio katika maeneo mahsusi ya Wilaya za Njombe na Makete ili wakulima waweze kupunguza umbali wa kuguata huduma hiyo.
Pamoja na hayo, ameliagiza kampuni la mbolea la PREMIUM AGROCHEM LTD kuongeza ukubwa wa eneo la kuhifadhia mbolea na kuongeza kiasi cha mbolea inayofikishwa mkoani humo ili kukidhi mahitaji ya wakulima kwa msimu wote wa kilimo.
Pamoja na kutembelea kampuni la OCP, Dkt. Ngailo ametembelea kampuni nyingine za mbolea ikiwa ni pamoja na YARA, MTEWELE, PREMIUM na Minjingu