Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
TFRA yapokea matokeo ya utafiti kuhusu uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini
13 Nov, 2024
TFRA yapokea matokeo ya utafiti kuhusu uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imepokea taarifa ya matokeo ya awali ya utafiti kuhusu matumizi ya makaa ya mawe na gesi asilia katika uzalishaji wa mbolea hususan zenye kirutubisho cha naitrojeni kutoka Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Mbolea (IFDC) chenye makao makuu yake nchini Marekani.  

Akizungumza mara baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema, Serikali imepokea maoni yaliyotolewa na watafiti ya kufungamanisha Taasisi za Serikali katika uvunaji wa malighafi zinazopatikana nchini kwa manufaa mapana ya nchi.

Amesema, kufuatia utashi wa kisiasa uliopo, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha uwekezaji kwenye viwanda unawezekana kwa kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kama barabara na reli na upatikanaji wa nishati ya kutosha.

Aidha, amesema TFRA itashirikiana na TPDC, GST na TIC ili kuwezesha matumizi ya malighafi zilizopo nchini katika uzalishaji wa mbolea na manufaa mengine kupitia wawekezaji watakaokuwa tayari kuwekeza.

Amesema, kwa sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wakulima kutumia mbolea ambapo ndani ya miaka miwili matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka takribani tani 360,000 hadi kufikia tani 840,000 na hivyo kutoa uhakika wa soko.

Ameongeza kuwa, uwepo wa malighafi za kuzalisha mbolea nchini ni fursa ya uwekezaji katika viwanda vya kuzalishaji mbolea ili kuhudumia soko la ndani na nchi zinazotuzunguka kutokana na nafasi nzuri ya kijiografia ya nchi yetu.

Akiwasilisha mada wakati wa warsha hiyo, Indrabhuwan Singh Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya MeTL amesema, Tanzania ina wigo mpana wa kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha mbolea kutokana na uwepo wa viwanda vichache vinavyozalisha mbolea nchini.

‘‘Nchi yetu ina wazalishaji wachache wa mbolea  ambao ni Yara, ITRACOM, Minjingu na wazalishaji wengine ambapo baadhi ya wazalishaji huchanganya mbolea kulingana na mahitaji ya udongo na mazao yanayolimwa." Singh alikazia.

Pia, amesema huu ni wakati muafaka kwa wadau wa mbolea, Serikali, Taasisi za Fedha na wawekezaji kushirikiana ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa kapu la chakula (food basketi) kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

‘‘Sote tutajivunia kuona wakulima wakitumia mbolea zinazozalishwa hapa nchini,’’Singh amekazia.

Kwa upande wake, mshauri elekezi wa IFDC kutoka ASNL Advisory Limited, Humphrey Simba amesema, utafiti uliofanyika unaonesha uwezo mkubwa wa nchi kujitosheleza kwa mbolea kutokana uwepo wa rasilimali zote muhimu za kuzalisha bidhaa hiyo ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe, gesi asilia na umeme wa kutosha.
Simba amesema, IFDC kwa kushirikiana na USA Sera Bora Project wamefanya utafiti kwa kupita kwenye migodi ya makaa ya mawe iliyopo mkoani Ruvuma ili  kujiridhisha na uwepo wa rasilimali hiyo ya kuzalisha mbolea.

"Lakini, pia tukapita kwenye miradi yetu ya gesi kule Mtwara na Songongo kuangalia kiwango cha makaa ya mawe, kuangalia kiwango cha gesi tulichonacho na namna ambavyo tunaweza tukatumia gesi na makaa ya mawe kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea." Simba aliongeza.

Amesema, mkutano wa leo ni kwa ajili ya kufanya wasilisho la awali kwa yale ambayo yamebainika ambapo miongoni mwa mambo yaliyojitokeza ni uwepo wa makaa ya mawe na gesi ya kutosha na hivyo kuwezesha kuendelea kufanya majadiliano ya kina na Serikali ili kujua endapo vyote viwili vinaweza kutumika kwenye uzalishaji wa mbolea.

IFDC ni shirika lisilo la faida linalolenga maendeleo endelevu ya kilimo na kuongeza usalama wa chakula duniani kwa kuongeza ufanisi wa matumizi ya mbolea, afya ya udongo, na uzalishaji wa mazao hasa katika nchi zinazoendelea.