Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

TFRA yaeleza sababu kusajili wakulima vijiji mashamba yaliko


Imeelezwa kwamba ili mkulima aweze kunufaika na ruzuku za mbolea zitakazotolewa msimu huu wa kilimo ni lazima awe amesajiwa kwenye ofisi yake ya kijiji.Lengo la usajili huo likiwa ni kuwatambua wakulima halisi kupitia viongozi wa vijiji yalipo mashamba yao na hivyo kuwa na taarifa sahihi za mkulima ikiwa ni pamoja na majina yake, ukubwa wa shamba, mazao anayolima, kitambulisho na hali ya shamba ikiwa ni la kukodi au lakwake mwenyewe.Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja Uagizaji na Uuzaji Mbolea nje ya nchi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Louis Kasera alipofanya ziara kwenye ofisi za maafisa kilimo wa miji na wilaya kwa lengo la kujiridhisha na mwenendo wa usajili wa wakulima kama ilivyoelekezwa na serikali.Louis amesema baada ya wakulima kujisajili katika vitabu vilivyofikishwa kwenye vijiji vyao, taarifa hizo zitaingizwa kwenye mfumo wa kidigitali utakaoonesha idadi ya wakulima na mahitaji ya mbolea kwa kila mkulima kulingana na taarifa walizojaza kwenye fomu hizo na hivyo kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wakati.Aidha, Louis amesema endapo itabainika mwenyekiti wa kijiji amemsajili mkulima hewa na asiyekuwepo kwenye eneo lake hatua zitachukuliwa dhidi yake.Louis aliendelea kufafanua kuwa kufuatia changamoto zilizojitokeza miaka ya nyuma ruzuku zilivyotolewa kwa mfumo wa vocha, serikali imeamua kuja na mbinu ya kuwasajili na kumtambua mkulima ni nani hivyo kuondoa changamoto ya kunufaisha watu wasiostahili kupata ruzuku hizo.Akijibu hoja ya Diwani wa Kata ya Mwembetogwa, Odo Chaula iliyodai kuna baadhi ya viongozi wa vijiji wamekataa kusajili wakulima wenye mashamba tofauti na maeneo wanayoishi, Afisa Biashara Doto Ditteba alisema mkulima yeyote anapaswa kusajiliwa na uongozi wa kijiji wa eneo ambako shamba lake lipo.Amesema ni vigumu kwa kiongozi wa kijiji kingine (unakoishi) kuthibitisha endapo kweli unamiliki shamba kijiji B kwani si eneo analolisimamia katika kutekeleza majukumu yake.Hata hivyo Diwani Chaula alieleza nia yake ya kuitisha mkutano ili kupitia maafisa kilimo wa Wilaya ya Makambako Mji waweze kutoa elimu kwa wananchi anaowasimamia juu ya taratibu za kujisajili ili wote waweze kuwa na uelewa wa pamoja katika kufanikisha upatikanaji wa mbolea za ruzuku.Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Makambako Mji Beatrice Tarimo alitoa shukrani kwa ujio wa viongozi kutoka TFRA na kukiri kuwa ujio wao umesaidia kuongeza uelewa wa namna sahihi ya utekelezaji wa agizo hilo.Pamoja na kutembelea eneo hilo wataalamu hao walitembelea Wilaya ya Mbalali, Njombe DC na Mafinga Mji na kukutana na DAICO wa maeneo hayo kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi la usajili.