TFRA yaweka mikakati usambazaji mbolea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imekutana na wadau wa Mbolea wa Mkoa wa Katavi kwa lengo la kufanya Tathmini ya hali ya usambazaji wa Mbolea Msimu wa kilimo 2023/2024 na kufanya maandalizi ya msimu mpya wa 2024/2025.
Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki kilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent kiliambatana na mafunzo kwa wafanyabiashara 52 waliohitimu mafunzo ya biashara ya mbolea na ambapo aliwatunukia vyeti.
Ameongeza kuwa, mafunzo hayo ni chachu kwa wafanyabiashara kuweza kutoa elimu/ufafanuzi kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na hivyo kuwawezesha wakulima kuongeza tija kwenye uzalishaji.
Laurent ameeleza umuhimu wa wakulima kuzingatia suala la kupima afya ya udongo kupitia maafisa ugani waliopo katika kata zao kwa kutumia vipima udongo vilivyotolewa na Serikali ili kutambua upungufu wa virutubisho vilivyopo katika udongo wanaoulima na kutumia mbolea sahihi.
Ameeleza kuwa, msimu wa kilimo 2024/2025 Serikali itatoa vishikwambi vitakavyosaidia zoezi la usajili wa wakulima kwa kuchukua alama za vidole, picha na majira ya nukta (GPS Coordinates) kulingana na ukubwa wa shamba na kutoa wito kwa wakulima kujitokeza kujiandikisha ili kutumia fursa ya ruzuku inayotolewa na Serikali.
Amesema, Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha misimu miwili 2022/23 na 2023/24 imetoa mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji kwa mkulima ili azalishe kwa tija, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza malighafi za viwanda.
Aidha, amewahakikishia wadau wa mbolea kuwa Serikali itaendelea kutoa Ruzuku ya Mbolea katika Msimu wa 2024/2025 na mbolea zote zitakuwa katika mfumo wa ruzuku.
Pamoja na hayo, amezielekeza kampuni za mbolea za ETG, OCP, Africian, Minjingu, TFC, Yara na nyinginezo kuhakikisha mbolea zinawafikia wakulima kwa wakati na kuwa na mawakala wadogo wadogo watakao fikisha mbolea hizo katika ngazi za Wilaya hadi Kata ili kuwawezesha wakulima kununua pembejeo hiyo muhimu pindi wanapouza mazao yao.
Mwisho, Laurent amezitaka Kampuni na mawakala wa mbolea kutii Sheria ya mbolea namba 9 ya mwaka 2009 na kueleza wakala au mkulima atakayekiuka au kuhujumu mpango wa ruzuku ya mbolea Serikali haitamvumilia.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Nehemia James akizungumza kwa N
niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi na Mshauri wa Kilimo Mkoa wa Katavi Faridi Mtilu aliwapongeza wadau wa mbolea kwa kuimarisha hali ya usambazaji wa mbolea mkoani hapo katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Amepongeza mpango wa TFRA wa kuja na kampeni maalumu ya kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kutumia mbolea kwa usahihi na kuwawezesha kuongeza tija ya uzalishaji, na kuwataka mawakala wa pembejeo za kilimo kuwaelekeze wakulima umuhimu wa kutumia mbolea katika kuingeza tija.
Ameeleza kuwa, Mkoa wa Katavi ni Mkoa wa kilimo ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wake ni wakulima.
Amebainisha kuwa, licha ya matumizi ya mbolea mkoani humo kuwa kidogo, unaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia maafisa ugani ili kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kutumia mbolea katika uzalishaji.
Ameiomba TFRA kushirikiana na Kampuni za Mbolea kuhakikisha msimu wa kilimo 2024/2025 mbolea zinafika kwa wakati kabla ya mwezi Septemba ili wakulima waweze kununua mbolea hizomapema.
Akihitimisha James amesema Mkoa wa Katavi utaendelea kusimamia kikamilifu zoezi la usajili wa wakulima pamoja na usambazaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima na kuwa mkoa umejiwekea Mpango Mkakati wa kuongeza matumizi ya mbolea kufikia zaidi ya tani 17,000 kwa mwaka.