TFRA kuimarisha usambazaji wa mbolea msimu ujao

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Seikali za Mitaa imesema imejipanga kuimarisha usambazaji wa mbolea nchini katika msimu wa 2023/2024.
Akizungumza katika nyakati tofauti katika mikoa Njombe na Ruvuma Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dkt.Stephan Ngailo amesema kutokana na changamoto za usambazaji wa mbolea zilizojitokeza katika msimu wa 2022/2023 Mamlaka imekuja na mikakati ya kuimarisha na kusogeza mbolea karibu zaidi na wakulima.
Dkt. Ngailo amebainisha kuwa mkakati wa kwanza unalenga kuwahamasisha wakulima kujisajili na kuhuisha taarifa zao mapema katika daftari na mfumo wa ruzuku ili kunufaika na mbolea ya ruzuku kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji Dkt.Ngailo ameambatana na wataalamu wa Mamlaka katika ziara inayolenga kufanya maandalizi ya msimu wa 2023/2024 hususan usambazaji wa mbolea.
Amesema kuwa mkakati mwingine ni kuainisha maghala ya serikali au watu binafsi yaliyo karibu na wakulima ambayo yatakuwa ni vituo vya mauzo ya mbolea ya ruzuku.Kaimu mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye ni Mkuu wa Mkuu wa Wilaya ya Songea Bwana Wilman Ndile amesema Mkoa wa Ruvuma ni moja ya mikoa inayozalisha kwa wingi hivyo suala la mbolea ni nyeti na linachulikuliwa kwa uzito mkubwa na wakulima.
Kutokana na umuhimu wa mbolea katika uzalishaji mkoani humo, tayari mkoa umeanza kuhamasisha wakulima na vyama vya ushirika kujisajili mapema ili kusambaza mapema kuanzia tarehe 1 mwezi Julai, 2023.
Amewataka wakulima kuondokana
na kasumba ya kununua mbolea wakati wa kupanda na badala yake wanunue wakati wanauza mazao
yao.
Katika msimu wa 2022/2023 Mkoa wa Ruvuma umetumia zaidi ya tani 75, 000 za mbolea na inategemewa kuongezeka katika msimu ujao, amesema Mkuu wa Wilaya.
Ndile amesema kuwa kutumia vyama vya ushirika kusambaza mbolea kwa wakulima ndio njia sahihi ya kuhakikisha kuwa wakulima wanapata pembejeo hiyo muhimu kwa wakati na tayari mkoa umeainisha maghala katika kila kata.