TFRA Kanda ya Kaskazini yamwagiwa sifa kwa utendaji

Wajumbe wanne wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) wameipongeza ofisi ya Kanda ya Kaskazini kwa utendaji mzuri pamoja na mahusiano mazuri baina yao na wadau anaoshirikiana nao katika utekelezaji wa majukumu yake.
Akiongea katika kikao baina ya watumishi wa TFRA wa kanda hiyo, mjumbe wa bodi Lilian Gabriel Peter amesema toka ziara ianze mkoani Tanga wameshuhudia kuwepo kwa mashirikiano mazuri baina ya TFRA na wadau wake ikiwa ni pamoja na watendaji wa serikali katika Ofisi za Mikoa, wafanyabiashara wa mbolea (mawakala), Waingizaji wa mbolea (importers) pamoja na wakulima ambao wote wanasifu ushirikiano wanaoupata kutoka ofisi ya Kanda.
“Hakika nimeuelewa msemo usemao kizuri chajiuza kibaya chajitembeza” Lilian alimaliza kusema.
Kwa upande wake Mjumbe Hadija Jabiri aliungana na mjumbe aliyetangulia kutoa pongezi kwa TFRA na kuongeza kuwa, kutokana na ushirikiano ambao mamlaka inautaka kutoka kwa mawakala wa mbolea huku akitolea mfano wakala wa Mbolea Sungura General Suppliers wa Wilayani Hai kuhusika kusambaza mbolea kwa wakulima kupitia kampuni la mbolea la TFC bila malipo kuwa ni vyema wadau hao wakatambuliwa na kupewa pongezi waazostahili.
Naye Mjumbe wa Bodi hiyo, Dkt. Shimo Peter Shimo alimpongeza Meneja wa Kanda na watendaji wote na kueleza kuwa ameonesha uwepo wake katika kusimamia tasnia ya mbolea katika kanda ya Kaskazini.
Alisema kufuatana na taarifa ya utekelezaji aliyoiwasilisha katika kikao hicho alitegemea kuelezwa kuwa ofisi yake ina watumishi ishirini lakini alistaajabu kuelezwa kuwa majukumu ya Kanda hiyo yenye mikoa minne na wilaya 32 inatekelezwa na watumishi watatu pekee.
“Kanda ni kubwa, inahitaji watumishi kiwango cha chini watano au sita lakini pamoja na uchache wenu mmefanya vizuri, nawapongeza sana” alikazia.
Pia, Mjumbe wa bodi Thomas Mwesiga ameeleza kuwa kanda inafanya kazi nzuri lakini pia inatimiza wajibu wake kama wadhibiti wa Mbolea na kuwataka kuendelea na moyo huo huo wa kusimamia malengo mazuri ya serikali.
“Meneja, tumefurahi kuwa na kiongozi ambaye yuko very aggressive katika kanda hii, lakini utambue kuwa haya mafanikio si ya kwako peke yako ni pamoja na watumishi wote wa kanda” Mwesigwa alisisitiza.
Aidha, Mwesiga aliwataka watumishi hao kujitahidi kuwa na taarifa za wadau wake wote na kueleza kazi ya udhibiti si ya kukaa ofisini ni ya kutembelea wadau, kujua changamoto zao na kuwashauri namna bora ya kuendesha biashara zao aidha kuelimisha juu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda, Gothard Liampawe amesema Kanda hiyo ni moja kati ya kanda tano za Mamlaka inayohudumia mikoa minne na wilaya 32.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara na kueleza kuwa kanda hiyo ina jumla ya watumishi 6 ambapo pamoja naye wapo wadhibiti ubora watatu (3), Afisa Usafirishaji pamoja na Msaidizi wa ofisi.
Ameeleza majukumu aliopangiwa kutekeleza kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kuwa ni pamoja na ukaguzi kwa wafanyabiashara wa mbolea 600, ukaguzi wa nguzo za kuzalishia na kuhifadhia mbolea mia sita, kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wafanyabiashara na kuwatunukia vyeti, kukutana na wakaguzi na wadau wa mbolea na kujadiliana changamoto mbalimbali za kiukaguzi na majukumu mengine kadri ya maelekezo ya serikali.
Aidha, alikiri kupokea maelekezo yote yaliyotolewa na wajumbe hao wa bodi na kuahidi kuyawasilisha kwenye menejimenti kwa ajili ya taratibu za utekelezaji kwa kanda yake na kanda nyingine za mamlaka hiyo