Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

TAARIFA KWA UMMA: BEI ELEKEZI KWA MBOLEA ZA KUPANDIA NA KUKUZIA KWA MSIMU WA KILIMO 2022/2023


1.0UTANGULIZI

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Authority - TFRA) kwa niaba ya Wizara ya Kilimo ina jukumu la kutoa bei elekezi ya mbolea ambapo wafanyabiashara wa mbolea wanatakiwa kuuza kwa bei elekezi au chini yake. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017.

Katika kutekeleza jukumu hilo la kisheria, TFRA imefanya mapitio ya bei elekezi kwa mbolea ya DAP na UREA katika kila kituo cha mauzo ambazo zitaanza kutumika tarehe 01 Desemba, 2022 (Bei zinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Kilimo, tfra na katika ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa Tanzania Bara). Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa mbolea inauzwa nchini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia tasnia ya mbolea.

  • 2.0MJENGEKO WA BEI ELEKEZI

Kwa kuwa mbolea za DAP na Urea zinazotumika nchini huingizwa kutoka nje ya nchi, na kwa kuwa Mamlaka imeratibu uingizaji wa mbolea hizo kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja (BPS), mapitio ya bei elekezi yamezingatia bei za zabuni, gharama za kuondosha mzigo bandarini na kusambaza hadi kumfikia mkulima. Hivyo, gharama za mjengeko wa bei elekezi ni kama ifuatavyo: -

  • i.Bei ya kufikisha mbolea hadi bandari ya DSM (CIF);
  • ii.Tozo za Mamlaka ya Bandari (TPA) na taasisi mbalimbali za udhibiti, gharama za kuondosha mzigo, vifungashio, kufungasha, usafirishaji hadi kwenye ghala la mwingizaji na kuhifadhi;
  • iii.Gharama za usimamizi na faida ya mwingizaji;
  • iv.Gharama za usafiri hadi kwa muuzaji wa rejareja na faida ya mfanyabiashara.

Serikali imeelekeza aina moja ya mbolea kuuzwa kwa bei inayofanana kwa wakulima nchini kote (pan territorial pricing). Hivyo, mapitio ya bei elekezi hayana athari kwenye bei ya mkulima ambapo mbolea ya DAP itaendelea kuuzwa kwa TZS 70,000, na Urea TZS TZS 70,000 baada ya kuweka ruzuku ya Serikali. Aidha,hakuna mfanyabiashara atakeye ruhusiwa kuuza mbolea nje ya mpango wa ruzuku. Hivyo, tofauti kati ya bei elekezi kwa kila eneo na bei ya mkulima italipwa na Serikali kama ruzuku kwa mkulima.

USIMAMIZI WA BEI ELEKEZI

Kwa kuwa mbolea zote zinauzwa katika mpango wa ruzuku, Serikali kupitia TFRA imesajili waingizaji na wazalishaji wa mbolea pamoja na mawakala wanaosambaza na kuuza mbolea kwa wakulima na kuwapa namba maalum za utambulisho. Hata hivyo, ili azma ya Serikali itimie ni muhimu kwa Mamlaka zote husika katika ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika namba ya uwakala na bei elekezi sehemu zinazoonekana kwa urahisi kwa wanunuzi. Pia ni vema mamlaka hizo zikasimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango wa ruzuku ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu uzingatiaji wa bei za mbolea ya ruzuku na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima katika maeneo husika.

  • 4.0UDHIBITI WA UTOROSHWAJI WA MBOLEA NJE YA NCHI

Pamoja na kwamba mpango wa ruzuku ya mbolea ni neema kwa wakulima, wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wanaweza kutumia fursa hiyo kuwalaghai wakulima na kununua mbolea kwa majina yao na baada ya hapo kutorosha mbolea kwenda nchi jirani. Hali hii itahatarisha utoshelevu wa mbolea kwa wakulima wetu na pia kuingizia hasara Serikali katika fedha inazotoa kama ruzuku kwa lengo la kumnufaisha mkulima na kuongeza uzalishaji nchini. Pamoja na uelimishaji ambao Serikali inaendelea kuufanya, ni vyema Mamlaka zote za Serikali zikashirikiana na wadau wote hususan katika mikoa ya mipakani kama Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Kagera, Kilimanjaro, Arusha na mikoa mingine kuhakikisha mbolea ya ruzuku haitoroshwi kwenda nchi jirani.

Vilevile, natoa onyo kali kwa wafanyabiashara wachache wenye tabia hizo au mpango wa kutorosha mbolea ya ruzuku kwenda nchi jirani kutothubutu kufanya hivyo kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao pindi itakapothibitika. Aidha, endapo kutakuwa na haja ya wafanyabiashara kuuza mbolea nje ya nchi, basi wafanye hivyo kwa kuzingatia sheria za nchi na sio kutorosha mbolea ya ruzuku.

  • 5.0HITIMISHO

Ni matumaini ya Serikali kuwa, mpango wa ruzuku ya mbolea utawezesha wakulima kutumia mbolea zaidi na hivyo kuongeza uzalishaji na tija kwa ajili ya utoshelevu wa chakula na kuzalisha malighafi ili kuimarisha uchumi wa viwanda. Hivyo, niwakumbushe wataalam na wadau wa kilimo kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati katika kuwaelimisha wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo. Aidha, natoa wito kwa Mamlaka zote katika ngazi za mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika usimamizi wa mbolea ya ruzuku ili Serikali ifikie azma yake na pia mkulima aweze kutumia fursa hii kubadilisha maisha yake kupitia kilimo.

bei elekezi 50 kg urea (30 novemba, 2022)

bei elekezi dap 50kg (30 novemba, 2022)

Dkt. Stephan E. Ngailo

MKURUGENZI MTENDAJI

Novemba 30, 2022