SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA KILIMO CHA TUMBAKU: WAZIRI BASHE AKABIDHI HUNDI YA BILIONI 13 KWA TCJE

Katika jitihada za kuimarisha sekta ya kilimo na kuongeza tija kwa wakulima, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), amekabidhi hundi ya Shilingi Bilioni 13 kwa Chama cha Ushirika cha Tobacco Cooperative Joint Enterprises Limited (TCJE).
Fedha hizo zinatolewa kama ruzuku kwa wakulima wa tumbaku ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mapato yao.
Hafla hiyo imefanyika tarehe 29 Januari 2025, katika Ukumbi wa Wizara ya Kilimo, jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Bashe amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya tumbaku, jambo ambalo limechangia ongezeko la pato la mkulima kutoka wastani wa Dola 1 ya Marekani hadi Dola 2.3 kwa kilo.
Aidha, uzalishaji wa tumbaku umeongezeka kutoka wastani wa tani 50,000 hadi tani 122,000 kwa mwaka, huku mapato ya wakulima yakifikia Dola za Marekani Milioni 269.
Amesema, ongezeko hilo limeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa tumbaku, nyuma ya Zimbabwe, huku mauzo ya nje yakivuka Dola za Marekani Milioni 400 kwa mara ya kwanza.
Mbali na sekta ya tumbaku, Waziri Bashe pia ameeleza maendeleo katika matumizi ya mbolea nchini. Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa ruzuku ya mbolea, matumizi ya mbolea yalikuwa tani 360,000 pekee.
Hata hivyo, kutokana na mpango huo, matumizi yameongezeka hadi tani 840,000 katika msimu wa kilimo uliopita, na lengo kwa msimu huu ni kufikia tani 1,000,000. Pia, matumizi ya mbolea kwa ekari yamepanda kutoka kilo 15 hadi kilo 24, huku Serikali ikilenga kufikia kilo 50 ifikapo mwaka 2030.
Hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta ya kilimo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata faida zaidi, uzalishaji unaongezeka, na Tanzania inasalia kuwa mchezaji mkubwa katika soko la kimataifa la mazao ya kilimo