Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Serikali kuendelea kutoa mbolea ya ruzuku hadi 2026
29 May, 2024
Serikali kuendelea kutoa mbolea ya ruzuku hadi 2026

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa serikali itaendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea nchini kwa kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima hadi mwaka 2025/2026 ili kuongeza matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 kwa hekta hadi kufikia kilo 50 kwa hekta.



Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2023/2024 jijiini Dodoma.



Waziri Bashe amesema serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea na usajili wa wakulima katika mfumo wa kidigitali ili kulifanya Taifa kuwa na uhakika wa takwimu na taarifa za wakulima.



Aidha, Waziri Bashe amesema serikali kupitia TFRA itaendelea kuratibu uingizwaji wa wa tani 750,000 za mbolea nchini.



Waziri wa Kilimo ameongeza kuwa Wizara yake itaiwezesha Kampuni ya Mbolea (TFC) kupata billioni 40 kama mtaji na hivyo kuongeza mtaji wa kampuni hilo na kuwa bilioni 46 kwa ajili ya kununua mbolea na kununua ardhi ya kujenga kiwanda cha kuchanganya mbolea kwa kushirikiana na sekta binafsi.
"Hatua hii inalenga kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kuimarisha upatikanaji wa mbolea kulingana na afya ya udongo ya eneo husika", alisema Waziri Bashe.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa mbolea Waziri Bashe amesema Wizara kupitia TFRA ilipanga kuratibu uingizaji, uzalishaji na usambazsji wa wa tani 650, 000 za mbolea kwa msimu wa 2022/2023 unaoishia mwezi Juni 2023.



Hadi kufikia Aprili 2023 upatikanaji wa mbolea umefikia tani 819,442 ikiwa ni asilimia 126 ya lengo
Kiasi hicho kimetokana na tani 75, 399 zilizozalishwa nchini, tani 617, 079 zilizoagizwa nje ya nchi na tani 126, 964 ikiwa ni bakaa ya msimu wa 2021/2022' alisema Bashe, na kuongeza kuwa hili ni ongezeko la asilimia 46 ikilinganishwa na msimu wa 2021/2022 ambapo upatikanaji wa mbolea ulikuwa tani 560, 551.