Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Rais Dkt. Samia azindua kadi janja ya Mkulima Nanenane Dodoma
10 Aug, 2024
Rais Dkt. Samia azindua kadi janja  ya Mkulima Nanenane Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua na kugawa Hati ya Hakimiliki Ardhi ya kimila pamoja na kitambulisho janja (farmer smart card) kwa wakulima waliokidhi vigezo.

Akiwa mkulima namba moja Mhe. Rais  amekabidhiwa kadi hiyo na Waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe na kuelezwa namna kadi hiyo inavyofanya kazi.

Akitoa maelezo kwa Mhe. Rais  kuhusu kadi hiyo,  Mkurugenzi  Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Bw. Joel Laurent amesema kuwa, kitambulisho hicho kimeunganishwa na mifumo mbalimbali kama vile NIDA, Ardhi, kadi ya Jamii, Benki na pembejeo za ruzuku kitakachomwezesha mkulima  kupata huduma mbalimbali za kifedha kama vile kutoa na kuweka fedha benki, kupokea malipo ya mauzo ya mazao ya mkulima, huduma za bima zikiwemo bima za afya, bima za pembejeo kwa atakayehitaji na kukidhi vigezo.

Bw. Laurent amesema, katika kutekeleza mpango wa Ruzuku ulioanzishwa na Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika msimu wa kilimo 2022/23, Wizara ya Kilimo kupitia TFRA kwa kushirikiana na wadau wa kilimo ilianzisha mfumo wa kidigitali wa usajili wa wakulima na usambazaji wa mbolea nchini Ili kurahisisha utoaji wa ruzuku ya Mbolea na kuifanya iwafikie walengwa ambao ni wakulima.

Amesema, mfumo huo unalenga kuhakikisha kuwa; Mkulima, eneo la uzalishaji, aina ya mazao yanayolimwa na kiasi cha mbolea kinachotumika vinatambulika.

Laurent ameongeza kuwa, katika kuhakikisha kuwa kuna taarifa sahihi za eneo la uzalishaji (shamba), Mamlaka inatekeleza mpango wa kuchukua majira nukta ya eneo la uzalishaji  yaani shamba  husika na kuingiza taarifa hizo katika mfumo huo wa usajili wa wakulima.

Aidha, katika kutekeleza azma ya Mhe. Rais ya kuhakikisha mifumo mbalimbali ya uendeshaji serikalini inasomana, Mamlaka imeanza mashirikiano na Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi ili kuunganisha mifumo ya usajili wa wakulima na mfumo wa matumizi bora ya ardhi.

Amesema kuunganishwa kwa mifumo hiyo kutamwezesha mkulima aliyesajiliwa na anayekidhi vigezo kuweza kupimiwa na kupatiwa Hatimiliki ya ardhi inayolenga kumsaidia kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo fursa za mikopo kwenye taasisi za kifedha.

Mkurugenzi Laurent  amesema, TFRA kupitia Wizara ya kilimo imefanikisha upatikanaji wa Hatimiliki ardhi kwa wakulima waliosajiliwa katika mfumo zitolewazo na Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi.

Mhe. Rais alikabidhi hati za umiliki wa ardhi kwa wakulima wawakilishi watano (5) waliotoka katika mikoa mbalimbali nchini wakiwemo pia wakulima kutoka katika maeneo yanayotekeleza mpango wa kilimo wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).