Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Kilimo

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA)

TFRA Logo
Rais Dkt. Samia afurahishwa na tija itokanayo na utekelezaji wa mbolea za ruzuku
09 Aug, 2024
Rais Dkt. Samia afurahishwa na tija itokanayo na utekelezaji wa mbolea za ruzuku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na tija iliyotokana na utekelezaji wa mbolea za ruzuku na kuitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuchapa kazi na kueleza kilimo kitatuinua.

Ametoa kauli hiyo Trehe 8 Agosti, 2024 alipotembelea banda la Mamlaka na kupokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo. Akizungumza kwa niaba ya wakulima wote nchini ndani ya banda la Mamlaka, Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo ametoa shukrani kwa maamuzi ya kutekeleza mpango wa mbolea za ruzuku kuanzia msimu wa kilimo wa 2022/2023 na 2023/2024, na kwa kukubali kuendelea kutoa ruzuku hiyo hadi msimu wa kilimo wa 2025/2026.

Amesema, mpango huo umekuwa na matokeo chanya kwa wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla. Akieleza tija iliyotokana na utekelezaji wa mpango huo, Dkt. Diallo amesema, tija ya uzalishaji imeongezeka kutoka tani 17,148,290 mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani 20,402,014 mwaka 2022/2023. Aidha, matumizi ya mbolea nchini yameongezeka kutoka tani 363,000 katika msimu wa kilimo wa 2021/2022 hadi kufikia tani 840,000 katika msimu wa kilimo wa 2023/2024.

Tunatarajia matumizi ya mbolea kuongezeka zaidi hadi kufikia tani 1,000,000 ifikapo mwishoni mwa msimu wa 2024/2025.Hii inazidi malengo ya Abuja yaliyowekwa na nchi za Afrika mwaka 2006, ambapo walikubaliana kuwa matumizi ya mbolea yafikie kilo 50 kwa hekta moja ifikapo mwaka 2025.

"Mheshimiwa Rais, mpango huu pia umetuwezesha kuwatambua wakulima na maeneo yao ya uzalishaji, tunakupongeza kwa juhudi hizi na tunatumaini kuwa mafanikio haya yataendelea kukua na kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika sekta ya kilimo na maisha ya wakulima nchini".

Dkt. Diallo aliongeza. Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amewataka wakulima ambao bado hawajasajiliwa au kuhakiki taarifa zao kufanya hivyo sasa ili wasipitwe na fursa hizo adhimu zinazotolewa kupitia kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku.

Mbolea Day