Ondoeni mbolea feki : Bashe aiambia TFRA

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA kuimarisha ukaguzi wa pembejeo hiyo nchini ili kuondoa mbolea zote zisizokidhi viwango.
Waziri Bashe amesema kuwepo kwa mbolea feki kwenye mnyororo wa uzalishaji kunapunguza tija kwenye shughuli za kilimo.
"Hatuwezi kuruhusu kuwepo kwa mbolea feki, pale anapopatikana muuzaji kuwa na mbolea feki kumpiga faini sio suluhisho, lazima tuwe wakali ni bora kumfungia biashara kama hawezi kufuata taratibu" Amesema Waziri Bashe.
Waziri Bashe ameyasema hayo leo tarehe 31 Machi, 2023 alipokuwa akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya TFRA ikiwa ni bodi ya nne tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2012.
Waziri Bashe ameitaka Bodi iliyoteuliwa kuhakikisha kuwa matumizi ya mbolea yanaongezeka kutoka Kilo 19 kwa hekta mpaka kufikia kilo 50 na kueleza ongezeko hilo litaleta matokeo chanya kwenye uzalishaji.
Aidha, ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inasimamia suala la usajili wa wakulima na hivyo kuwezesha uwepo wa kanzi data inayowatambua wakulima wote nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dkt. Antony Diallo ametoa shukrani zake kwa niaba yake na wajumbe wote wa bodi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya kuisimamia na kuishauri Mamlaka yenye dhamana nchini.
Aidha, Dkt. Dialo ameahidi kuwa, bodi yake itafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa tasnia ya mbolea inatatua changamoto za wakulima na hivyo kuleta manufaa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Amesema, yeye na bodi yake wataisoma sheria ya mbolea pamoja na Mpango Mkakati wa Taasisi ili waweze kuyaelewa na kuyasimamia vyema majukumu waliyopewa.
Kufuatia wito wa Waziri Bashe wa kuondoa bidhaa feki kwenye sekta ya kilimo, Dkt. Diallo amesema bodi yake kwa kushirikiana na Menejimenti ya TFRA watakuwa macho sana kuhakikisha kuwa malalamiko ya wananchi yatokanayo na mbolea feki yanapungua.