Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Mwekezaji kutoka Slovakia kujenga kiwanda cha mbolea Pwani


Mwekezaji kutoka nchini Slovakia kupitia kampuni la ROKOSAN ameonesha nia ya kujenga kiwanda cha mbolea katika eneo la Soga Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Mwekezaji huyo Dkt. Adam Seo’ke ambaye aliambatana na wadau wengine kutoka makampuni mawili ya hapa nchini KOM na Selphina ameonesha nia yake wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) jijini Dar es Salaam leo tarehe 24 Mei, 2022 na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka Dkt.Stephan Ngailo

Akizungumza wakati wa kikao hicho Dkt Ngailo amesema matumizi ya mbolea kwa Tanzania yamepungua kutokana na bei ya bidhaa hiyo kuwa juu kiasi ambacho wakulima wadogo wanashindwa kumudu gharama ya bidhaa hiyo.

“Ujenzi wa kiwanda cha mbolea mkoani Pwani ni habari njema kwa wakulima wa Tanzania kwani utaongeza uzalishaji wa ndani na hivyo kumpunguzia mkulima makali ya kununua bidhaa hiyo kwa bei kubwa ambayo wengi wao hawawezi kumudu” Alisema Dkt.Ngailo.

Wawekezaji wakifuatilia maelezo ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo (hayupo pichani) kushoto ni Dkt. Adam Seo'ke, akifuatiwa na Stefan Seo'ke

Amesema maono ya serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha mbolea Afrika Mashariki na Kati na kuwahakikishia wawekezaji hao kuwa soko la bidhaa hiyo nchini ni la uhakika na kueleza pindi itakapotosheleza kwa matumizi ya ndani ya nchi itauzwa nchi jirani kama vile Demokrasia ya watu wa Kongo (DRC), Burundi, Uganda, Rwanda na nchi nyinginezo.

Pamoja na hayo, Dkt. Ngailo aliwahakikishia wawekezaji hao ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha hazma yao ya kuwekeza kwenye kiwanda cha mbolea inatimia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa uzalishaji wa ndani na ununuzi wa mbolea kwa pamoja Joseph Charos aliwashauri wawekezaji kuwekeza katika kuitangaza bidhaa watakayozalisha kwa vitendo kwani upatikanaji wa wateja utatokana na namna walivyoielewa bidhaa husika.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe walioshiriki kikao hicho kutoka kwa wawekezaji hao Dr. Adam Seo’ke amesema kiwanda wanachotarajia kukijenga kitakuwa kikizalisha mbolea ya asili ya kimiminika (organic folier fertilizer) na kuuzwa kwa bei nafuu kwani itazalishwa kwa kutumia malighafi za asili.

Amesema, ujenzi wa kiwanda hicho utafungua fursa za ajira pamoja na kuwahakikishia watanzania uhakika wa chakula kutokana na mbolea hiyo kuongeza virutubisho vya kutosha kwenye udongo pasipo kuwa na athari zozote kwenye afya za walaji.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo (wa pili kutoka kulia mbele) akiwa katika picha ya pamoja na wawekezaji waliofika kueleza nia ya kutaka kujenga kiwanda cha mbolea Mkoani Pwani.


Aidha, Adam ameomba ushirikiano baina yao serikali na taasisi zinazosimamia tasnia ya mbolea ambapo alihakikishiwa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka TFRA pamoja na taasisi nyingine serikalini.

Ujio wa wawekezaji wa kiwanda cha mbolea ni moja kati ya mikakati ya TFRA katika kuhakikisha uzalishaji wa ndani unaongezeka na hivyo kupunguza changamoto ya bei na upatikanaji wa mbolea nchini.

Tanzania Census 2022