Mkuu wa Wilaya ya Rorya aahidi kushirikiana na TFRA kutoa elimu ya mbolea
Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma I. Chikoka amesema atashirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), kuhakikisha anabadilisha mitazamo ya wananchi wake kwenye matumizi ya mbolea ili kuwawezesha kuongeza tija kwenye mavuno.
Chikoka amesema hayo tarehe 05 Agosti, 2024 alipokuwa akizungumza na Mwenyekiti wa bodi ya TFRA na watumishi wa Mamlaka hiyo waliofika ofisini kwake kueleza mpango wao wa kuelimisha umma kupitia kampeni maalumu ya "Kilimo ni mbolea" unaoendelea katika wilaya hiyo na maeneo mengine nchini.
"Mimi ni muumini wa matokeo napenda kuona hiki kinachofanywa na serikali kinaleta matokeo chanya kwa wananchi kwa kuongeza mavuno na kipato kutokana na matumizi sahihi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.
Amesema, kuna tija na matokeo chanya kwa watu wake endapo watatumia mbolea na kueleza kuwa anaunga mkono juhudi za Mamlaka za kuhakikisha kuwa jamii zetu zinabadilika sababu kilimo sasa hivi ni biashara.
"Sasa unaposema kilimo ni biashara na hutumii mbolea hapo inakuwa changamoto sana" Chikoka alikazia.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo amesema Matumizi ya hovyo ya ardhi ndio yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu ardhi.
Amesema, ongezeko la binadamu na uharibifu wa mazingira haviendani kabisa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kilimo kwenye miinuko kilizingatia kontua.
Aliongeza kuwa, ukataji wa miti ili kuongeza eneo la kilimo ni uharibifu mkubwa wakati unaweza kulima eneo dogo kwa mbolea ukavuna mazao mengi ya kutosheleza mahitaji na ziada.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Kanda ya Ziwa, Michael Sanga amesema Mamlaka imeamua kufanya kampeni katika eneo hilo kutokana na eneo hilo kuwa na matumizi hafifu ya pembejeo mbolea.