Mkuu wa Mkoa wa Kagera awataka wakulima kuacha kilimo cha mazoea
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amewataka wakulima mkoani humo kuacha kilimo cha mazoea kwa kuanza kutumia tekinolojia mbalimbali ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea katika shughuli zao za kilimo ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi.
Amesema yeye ni mkulima wa mpunga mkoani Morogoro na kwamba amelima ekari 12 na kuvuna gunia 400 za mpunga ambazo ni sawa na gunia 33 kwa ekari moja. Wakati Kipato kitokanacho na mavuno hayo endapo bei ya gunia itakuwa nzuri ni hadi milioni 40 na hivyo kuwasishi wana Kagera kuona wivu na kuona fursa wanayoipoteza kwa kutokutumia mbolea.
Mkuu wa Mkoa Mwassa ameyasema hayo leo tarehe 14 Agosti, 2024 alipokuwa akizungumza na wakulima wa Mkoa wa Kagera wakati wa ufunguzi wa kampeni ya "Kilimo ni Mbolea" inayolenga kuelimisha umma kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha usajili wa wakulima kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea.
Amewataka wakulima kujitokeza kujisajili kwenye mfumo ruzuku ya mbolea ili waweze kununua pembejeo hiyo kwa bei nafuu kwa kuwa Serikali imeweka imeweka ruzuku inayotolewa kwa wakulima kupitia mfumo huo.
Sambamba na uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa Mwassa amezindua shindano la usajili wa wakulima kwa wilaya zote za mkoa wa Kagera na kueleza Wilaya itakayoibuka mshindi kwa kusajili wakulima wengi ifikapo Desemba 2024 itazawadiwa.
Pamoja na hayo, amewataka maafisa ugani wa Kila Halmashauri kutumia vizuri vifaa vya kupima udongo vilivyotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ili kuwawezesha wakulima kutumia mbolea kuendana na uhitaji wa udongo wanaolima.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo amesema, mkulima anayetumia mbolea anapata mara kumi zaidi ya yule asiyetumia mbolea kwa kuwa anaweza kulima eneo dogo na kuvuna zaidi tofauti na mkulima anayelima eneo kubwa bila kutumia mbolea maana anatumia nguvu kubwa kwa mavuno kidogo.
Amesema kwa Mwaka Huu Mamlaka inajikita katika kuhamasisha matumizi ya mbolea kwenye zao la migomba na kahawa ili kuongeza tija ya uzalishaji kwenye mazao hayo ambayo ndio mazao makuu katika Mkoa huu.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Viongozi wa juu wa Mkoa wa Kagera, Wilaya, kata na vijiji, wakulima wa Wilaya ya Missenyi pamoja na kampuni za mbolea za Itracom na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC).