Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Mgumba aiagiza TFRA kuwasaidia wakulima kupata mbolea kwa mkopo.


Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba ameitaka Mamlaka ya Mbolea Tanzania kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuandaa Mfumo wa ugharamiaji wa Mbolea ili kumwezesha Mkulima kupata Mbolea kwa Mkopo mwanzoni mwa Msimu wa kupanda mazao na kulipa mkopo huo baada ya kuvuna Mazao yake.

Waziri Mgumba ametoa agizo hilo Octoba 13 mwaka huu katika maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Dakawa Mvomero Mkoani Morogoro ambapo alikuwa Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akizungumza na wakulima, Mashirika ya usambazaji wa Mbolea Tanzania katika siku ya maadhimisho ya Mbolea Duniani yaliyofanyika Dakawa Mvomero.

Aidha, kupitia maadhimisho hayo amelitaka Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kutoa taarifa ya afya ya udongo kwa wakulima na wadau wengine ili mtumiaji mbolea awe na uelewa wa mbolea ipi inatakiwa kutumika katika udongo wa aina gani hivyo kuwa na matumizi sahihi ya mbolea.

“Serikali imeshamaliza kufanya tafiti za udongo katika Mikoa yote 26, na sasa tumeanza tena kufanya awamu ya pili kwenye ngazi za Kata, lengo letu kila mtu kwenye kata yake afahamu ardhi aliyokuwa nayo ina afya gani, inakubali zao gani, aina gani ya mbolea inayohitajika ili kupata matumizi ya mbolea sahihi” alisema Waziri Mgumba.

Sambamba na maagizo hayo, Waziri Mgumba ametoa wito kwa Makampuni na wasambazaji wa mbolea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea na kufungua mashamba darasa karibu na mashamba ya wakulima ili kuwasaidia kutambua faida inayotokana na matumizi ya mbolea kutokana na wakulima wengi kutokuwa na elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea ambapo baadhi yao wamekuwa wakidai kuwa mbolea inaharibu udongo.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akitoa tuzo kwa wasambazaji wa mbolea Tanzania katika sikukuu ya kuadhimisha siku ya Mbolea duniani iliyofanyika Dakawa Mvomero Mkoani Morogoro.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TFRA Pro. Anthony Mshandete amesema katika awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania shirika hilo limefanikiwa kuimarisha mfumo wa uthibiti wa mbolea kwa kuhakikisha wakulima wamepata mbolea bora kwa wakati wote kuongeza upatikanaji wa mbolea ambapo mwaka 2015/2016 upatikanaji ulikuwa Tani 427,466 na mwaka 2019/2020 upatikanaji wa mbolea ulikuwa zaidi ya Tani 500,000.

Kwa upande mwingine, amesema TFRA inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo utegemezi wa mbolea kwa 90% kutoka nje ya nchi, utoroshaji wa mbolea mipakani na ushiriki hafifu wa vyama vya ushirika katika mfumo wa ununuzi wa Mbolea kwa pamoja - BPS.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akipokea zawadi zilizotolewa na Shirika la usambazaji wa Mbolea Tanzania katika maadhimisho siku ya Mbolea duniani yaliyofanyika Dakawa Mvomero Mkoani Morogoro. Picha Octoba 13 Mwaka huu.

Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akipokea zawadi zilizotolewa na Shirika la usambazaji wa Mbolea Tanzania katika maadhimisho siku ya Mbolea duniani yaliyofanyika Dakawa Mvomero Mkoani Morogoro. Picha Octoba 13 Mwaka huu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema kufanyika kwa mahadhimisho ya siku ya mbolea duniani kitaifa katika Mkoa huo umetoa hamasa na fursa kwa Wakulima Mkoani humo kukutana na wasambazaji wa mbolea na watafiti mbalimbali kupata elimu sahihi, kubadilishana mawazo, na kupewa maelekezo mazuri juu ya matumizi ya mbolea.

Sanare amesema Mkoa wa Morogoro ni ghala la chakula ambapo Mkoa huo umeweka mikakati ya kujipanga vizuri kutumia fursa ya Reli ya mwendo kasi (SGR) katika kusafirisha, kuuza na kununua bidhaa tofauti ambazo zitakuwa zinapatika Mkoani humo kwenda Mikoa mingine hapa nchini.

Pia, amesema Mkoa wa Morogoro umejipanga kuhakikisha unakuwa na zao linalotambulisha Mkoa huo kama ilivyo kwa Mikoa mingine ambapo zao kuu litakuwa Mpunga ambao utakuwa tofauti na sehemu nyingine katika Mikoa yote ya Tanzania.

“Mchele unaotokana na Mpunga hapa Morogoro utakuwa ni wa aina yake, hata leo mtaonja kidogo msizoee kukaa sana mnaotoka nje ya Mkoa, kuna aina mbalimbali ya mchele hapa, upo unaoitwa tukale na bwana…” alisema Sanare.

Siku ya Mbolea duniani huadhimishwa kila mwaka Oktoba 13 ikiwa ni kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi aina ya amonia kinachopatikana hewani, uvumbuzi huu uliofanywa na bwana Fritz Haber mwaka 1908.

Siku hii inalenga kuhamasisha wadau wa tasnia ya Mbolea duniani kote kuhusu kutekeleza jukumu lao kubwa katika kuhakikisha wakulima wanatumia mbolea bora na kwa usahihi ili kuleta mapinduzi ya kijani, hivyo kuwa na uhakika wa chakula.