Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Mfumo wa mbolea za ruzuku usijadiliwe kisiasa- Waziri Bashe


Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mfumo wa mbolea za ruzuku usijadiliwe kisiasa kwani Umewekwa mahsusi kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu kwa kupata takwimu za wakulima na kuweka kanzidata ya kukiendeleza kilimo nchini.


Amesema, aono ya nchi ni kuzalisha chakula kutosheleeza mahitaji ya nchi na kulisha nchi nyingine barani Afrika huku akitoa mfano wa 10% ya uzalishaji wa zao la mahindi na 15% ya zao la mpunga kulisha nchi nyingine barani Africa.

Waziri Bashe ameyasema hayo tarehe 19 Januari, 2023 alipokuwa akizungumza na wadau wa kilimo katika kiwanda cha kuchakata zao la parachichi Eatfresh kilichopo katika kijiji cha Tagamenda, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa mkoani Iringa katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo iliyolenga kufuatilia masuala ya kilimo nchini.

Waziri Bashe ameongeza kuwa, Mwaka huu hakutakuwa na upungufu wa uzalishaji kwa sababu ya changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwani matumizi ya mbolea yameongezeka ukilinganisha na miaka iliyopita.

Akizungumzia changamoto zilizojitokeza katika utoaji wa mbolea za ruzuku msimu huu waziri Bashe amesema, zimesababishwa na mwitikio mkubwa wa wakulima kusababisha usambazaji wa mbolea kutokuwa kama msimu uliopita ambapo zitaendelea kufanyiwa kazi kwa kuongeza vituo vya mauzo.

Akitoa takwimu za matumizi ya mbolea kwa mwaka 2022 Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Iringa amesema msimu wa kilimo wa 2021/2022 kiasi cha tani 19,000 kilitumika wakati msimu wa Mwaka 2022/2023 ambao ndio upo katikati kiasi cha tani 22,000 kimetumika na kueleza makadirio ni kutumia kati ya tani elfu thelathini hadi tani elfu arobaini kulingana na mwitikio wa wakulima kutumia mbolea.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni la Mbolea la Yara Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Andrew Ndundulu amesema, msimu wa kilimo uliopita yaani 2021/2022 kampuni yake iliuza kiasi cha tani 8,400 za mbolea na msimu huu wa 2022/2023 mpaka mwezi Januari wameuza kiasi cha tani 10,913 huku wakitarajia mauzo kufikia tani 13,000 au zaidi.