Mavunde: Ruzuku ya mbolea itawapunguzia wakulima mzigo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri wa Kilimo Antony Mavunde amesema kuwa serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 150 za ruzuku yambolea ili kuwapunguzia mzigo wakulima napia kuendelea kuvutia wawekezaji wajitokeze kuwekeza katika maeneo mbalimbali.
Mavunde amesema hayo wakati akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji walipotembelea kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Itracom Fertilizer Limited tarehe 23.06.2022 kilichopo jijini Dodoma, ambacho kimefanya uwekezaji wa Sh billion 180 katika eneo la Nala jijini humo.
Mavunde alisema hivi sasa taifa linakwenda kuondoa changamoto ya mbolea nchini, ambayo iko duniani kote kutokana na bei ya bidhaa hiyo kupanda kwa kiasi kikubwa mara kwa mara.
Mavunde alisema kwa kiwanda hicho cha mbolea kitasaidia upatikanaji wa mbolea ndani ya nchi ambao utakuwa ni tani 600,000 za mbolea kwa mwaka lakini pia tani 300,000 kwa mwaka za Chokaa ambapo uzalishaji huu utaanza mapema mwezi julai 2022.
Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji, Christine Ishengoma (katikati) wakati ilipotembelea Kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Intracom kilichopo Nala jijini Dodoma, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Itracom Nduwimana Nasaire
Alisema ujenzi wa kiwanda hicho utatatua changamoto mbalimbali ikiwemo kupanda kwa bei ya mbole kwa sababu uzalishaji utakuwa unapatikana hapa hapa nchini na wakulima watakuwa wanapata mbolea kwa wakati.Mavunde alisema moja ya changamoto ambayo inawakumba wakulima ni pembejeo kuchelewa, lakini kupitia utaratibu huu na kupitia kiwanda hicho serikali itatatua changamoto hizo kwa wakulima.
Alifafanua kuwa mbolea itakayozalishwa na kiwanda hicho ni Organo Mineral inayotumia samadi,kitendo ambacho kitatoa fursa kwa wafugaji kuweza kupeleka mbolea zao kiwandani hapo, jambo ambalo litasaidia kukuza uchumi wa Tanzania.
“Hivi sasa tunakwenda kutatua changamoto ya suala la Mbolea kwa wakulima, serikali itaendelea kuvutia wawekezaji ili kuhakikisha inamsaidia mkulima wa Tanania,”alisema Mavunde.
Mavunde alifafanua zaidi ya kuwa katika hatua za muda wa kati na mrefu mojawapo ni serikali kutenga fedha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo ya mbolea ili kuwapunguzia mzigo wakulima lakini hatua ya muda mrefu ilikuwa ni kuvutia wawekezaji ili waje kuwekeza hapa nchini.
Hata hivyo alimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan baada ya ziara ya Bururundi aliwavutia wawekezaji hao, kuja kuwekeza hapa nchini ambapo waliitikia wito na leo tunashuhudia uwekezaji mkubwa wa zaidi ya sh billion 180 katika hatua ya awali umefanyika hapa nchini.
Akizungumza mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Itracom Nduwimana Nasaire aliishukuru Kamati ya Bunge kuja kutembelea kiwanda hicho kwani wao kama wawekezaji wanatiwa moyo.
Akizungumia kuhusu uzalishaji, Nasaire alisema wanatarajia kuanza uzalishaji mwezi Julai, 2022ambapo wataanza na mbolea aina ya Organo Mineral ambayo tayari imefanyiwa utafiti na vituo vya utafiti hapa nchini na kuonyesha matokeo mazuri katika mazao ya maharage, mahindi, mtama na mpunga.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji Bi. Christine Ishengoma alisema kamati hiyo imefurahishwa na uwekezaji unaofanywa huku akiwataka wawekezaji hao kuhakikisha wanaanza kuzalisha mbolea hiyo kwa muda uliopangwa ili wakulima waanze kuitumia katika msimu ujao wa kilimo.