Matumizi ya mbolea kufikia kilo 50 kwa ekari ifikapo Mawaka 2050
Imeelezwa kwamba matumizi ya mbolea nchini yapo chini ikiwa ni wastani wa kg 20 hadi 22 kwa ekari ukilinganisha na malengo ya kufikia kg 50 kwa ekari ulioainishwa kwenye mpango wa mageuzi ya kilimo Afrika ifikapo mwaka 2050.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt.Hussein Mohamed tarehe 13 Oktoba, 2024 alipokuwa akihutubia kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani Babati mkoani Manyara.
Amesema, Matumizi ya mbolea ni muhimu katika kuhakikisha kuwa tunanufaika ipasavyo na udongo katika maeneo tunayolima, tunaongeza tija na kuboresha Maisha ya wakulima nchini.
Amesema mbolea ina mchango mkubwa katika kuongeza usalama wa chakula na ukuaji wa Uchumi nchini.
Akizungumzia manufaa ya uwepo wa mpango wa mbolea za ruzuku, Dkt. Hussein Mohamed amesema, mpango huo umewezesha kuongeza kwa matumizi ya mbolea nchinikutoa tani 363,509 mwaka 2021/2022 nakufikia tani 840,714 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la asilimia 131.2.
Aidha, amesema uwepo wa mpango huo umepelekea ongezeko la upatikanaji wa mbolea kutoka tani 560,551 mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani 1,213,729 mwaka 2023/24.
Amezielekeza TFRA na Mamlaka ya Mbegu Taasisi (TOSCI) kushirikiana na Secretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa kuendelea kuhamasisha wakulima kujisajili kwenye daftari ya wakulima ili kupata namba watakazozitumia kunufaika na mpango wa ruzuku ya mbolea na mbegu.
Pamoja na hayo, amezitaka taasisi hizo kusimamia kikamilifu Mpango wa utoaji wa ruzuku ya mbolea na mbegu kwa waulima na kuchukua hatua kwa yeyote atakayethibitika kuhujumu mpango huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema Mamlaka itahakikisha inashirikiana na Sekta binafsi kuhakikisha mbolea zinapatikana kwa wakati na kwa bei himilivu.
Awali akielezea maadhimisho ya siku ya Mbolea Duniani, Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, TFRA iliona ni vema kuongeza siku za maonesho ya Mbolea, kuwakutanisha wakulima na wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa tasnia ya mbolea ili kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, kujifunza teknolojia za kisasa na huduma mbalimbali zinazotolewa na wadau kwenye mnyororo wa thamani wa mbolea.
Amebainisha kuwa, Mamlaka imeendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mbolea ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea zenye ubora wakati wote.
Tanzania imeadhimisha siku ya Mbolea Duniani kwa mara ya sita mfululizo yakitangulia maonesho ya Mbolea na Kongamano la kwanza la Mbolea ikiwa na kauli mbiu " Tuongee Mbolea, Kilimo ni Mbolea" ikiakisi majukumu makuu ya mamlaka kuhakikisha mbolea bora inapatikana wakati wote kwa bei himilivu.