Matumizi Vyama vya Ushirika kusambaza mbolea kwamkosha Katibu Tawala Geita, Prof. Kahyarara
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Prof. Godius W. Kahyarara amepongeza uamuzi wa Serikali wa kutumia vyama vya ushirika katika kusambaza mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024.
Amesema, Vyama vya ushirika viko kwa wananchi na vinajua changamoto za wakulima na namna ya kuzitatua hivyo vitasaidia sana kupunguza malalamiko ya wakulima.
Katibu Tawala Prof. Kahyarara alitoa kauli hiyo tarehe 5 Juni, 2023 ofisini kwake akiwa katika kikao kifupi baina yake na timu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku Louis Kasera.
Aidha, Prof. Kahyarara aliiomba TFRA kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya mbolea vya ndani ili kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kueleza uzalishaji wa ndani utaongeza ufanisi zaidi katika kukuza kilimo na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni katika kuagiza mbolea nje ya nchi na baadaye kukuza uchumi wa nchi.
"Lazima tujitosheleze kwa chakula, mbolea, viuwatilifu, utafiti na gesi ili kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye mfuko wa taifa", Kanyarara alikazia.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku, Louis Kasera alieleza lengo la kufika mkoani hapo kuwa ni pamoja na kuhamasisha watendaji kuendelea na zoezi la usajili na uhuishaji wa taarifa za wakulima ili kuwawezesha kunufaika na mbolea za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2023/2024.
Alisema, serikali imejipanga kutumia Vyama vya Ushirika kufikisha mbolea kwa wakulima na kubainisha kuwa, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itasaidia kufikisha mbolea kwenye maeneo yasiyofikika na hivyo kuwawezesha wakulima kutokwenda zaidi ya Kilomita 15 kufuata pembejeo ya mbolea.
Aidha, Kasera alieleza kuwa, ifikapo tarehe mosi Julai mbolea zitakuwa zimefikishwa karibu na wakulima na kutoa wito kwa wakulima kujitokeza kununua mbolea na kupunguza misururu mirefu wakati wa msimu.
"Nguvu kubwa tunataka kuweka kwenye vyama vya ushirika na kueleza Chama Kikuu cha Ushirika cha Tarime (WAMAKU) kilisaidia sana katika kusambaza mbolea msimu uliopita katika maeneo ya Tarime na Serengeti na hivyo serikali ikaona ni vyema kutumia vyama hivyo ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wakulima.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Geita, Dkt. Elfas Mseya aliishukuru TFRA kwa kuanza mchakato wa maandalizi ya msimu wa kilimo mapema na kueleza hii itasaidia kupunguza changamoto za misururu mirefu ya kununua mbolea kwa mawakala.
Aidha, ameipongeza TFRA kwa kukutana na watendaji katika kata za mikoa na wilaya kwani itawapa wepesi katika kusimamia mchakato mzima wa kusajili, kuhuisha na kusimamia usambazaji wa mbolea kwa wakulima.