Bodi mpya ya Wakurugenzi TFRA yapongezwa kusikiliza changamoto za mawakala wa mbolea
Mawakala wa usambazaji wa Mbolea mkoani Kigoma wameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuanza majukumu yao kwa kusikiliza changamoto za wadau ili kuzipatia ufumbuzi.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 21.07.2023 wakati wa kikao kazi cha pamoja cha bodi hiyo na mawakala wa mbolea wapao 50 pamoja na vyama vya ushirika mkoani humo.
Aidha wadau hao wamempongeza Meneja wa Kanda ya Kati wa TFRA Joshua Ng'ondya kwa utendaji na mahusiano mazuri na mawakala katika mkoa wa Kigoma na kurahisisha utekelezaji wa mpango wa ruzuku katika msimu wa 2022/2023. Akizungumza kwa niaba ya mawakala mkoani Kigoma Mwenyekiti wa Mawakala mkoa wa Kigoma Yoram Kalosa amesema Hatua ya bodi mpya kuamua kutoka ofisini na kwenda kusikiliza kero na changamoto za wadau inastahili kupongezwa kwani wakulima wengi wako vijijini na sio mjini.
Kalosa amesema changamoto kubwa walizozipata katika msimu uliopita ni pamoja na uchache wa vituo vya mawakala jambo ambalo lilisababisha wakulima kusafiri umbali mrefu na hivyo kuwaongezea gharama za uzalishaji.
Aliongeza pia kuwa mfumo wa kidigitali wa utoaji wa mbolea za rukuzu katika msimu uliopita ulileta usumbufu kwa mawakala na wakulima hivyo wameiomba serikali kuhakikisha kuwa maboresho ya mfumo yanafanyika kabla msimu mpya wa kilimo haujaanza.
Wadau wameiomba pia Bodi ya TFRA iingilie kati suala la makampuni makubwa kuwabana mawakala wadogo kuuza mbolea ya kampuni moja tu badala ya kuwapa uhuru wa kuuza mbolea za makampuni yote wanayoyataka.
Wemeongeza kuwa katika msimu uliopita mawakala wadogo wengi walikuwa na changamoto ya mitaji midogo na hivyo kushindwa kuchukua mzigo kwa mawakala wakubwa au makampuni kwa fedha taslim
Awali akifungua kikao kazi hicho Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Dkt. Anthony Diallo aliwaeleza kuwa bodi yake ni mpya hivyo imekuja kujifunza na kuwasikiliza moja kwa moja wadau wa mbolea katika Kanda ya Kati na Ziwa.
Dkt.Diallo alisema kuwa Mamlaka inatambua mchango mkubwa wa mawakala wa usambazaji wa mbolea nchini kwani wao ndio wanamfikishia mkulima pembejeo hiyo muhimu kwa wakati.
Alisema mkoa wa Kigoma una ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo hivyo matumizi ya mbolea yataongeza uzalishaji wenye tija na hivyo mkoa kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada katika nchi jirani.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati TFRA Joshua Ng'ondyaamesema kuwa Mamlaka inaendelea kufanya usajili wa wakulima wote kupitia mfumo mpya ulioboreshwa ili wafanyabiashara pamoja na vyama vya ushirika viweze kunufaika na faida ya kuuza mbolea ya ruzuku kwa wakulima.
Amesema tayari kanda yake imetoa mafunzo kuhusu mfumo wa uuzaji wa mbolea za ruzuku kwa vyama vya ushirika 226 na baadaye vitasajiliwa kuwa mawakala wa usambazaji wa mbolea