KONGAMANO LA KWANZA LA MBOLEA
Bilioni 300 imetengwa kugharamia ruzuku ya mbolea nchini- Mweli
Imeelezwa kwamba, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 300 kwa mwaka wa fedha 2024/25 ili kugharamia ruzuku ya mbolea kwa wakulima.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Mbolea linalofanyika tarehe 11 na 12 Oktoba, 2024 katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Kongamano hilo lililoratibiwa na Mamalaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) limehusisha uzinduzi wa Mkakati wa Mbolea utakaosaidia katika uendelezaji wa Tasnia ya Mbolea nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Katibu Mkuu Mweli amesema Serikali imeendelea kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini kwa kuwezesha utoaji wa ruzuku ya mbolea kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2024/25.
Kongamano hilo la siku mbili ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani inayoadhimishwa tarehe 13 Oktoba kila mwaka ambapo mwaka huu inaadhimishwa nchini kwa mara ya sita.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2024/25 ni ''Tuongee Mbolea, Kilimo ni Mbolea", yakiwa yamewakutanisha wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mbolea kutoka ndani na nje ya nchi.
Wadau hao ni pamoja na watunga sera, wazalishaji wa mbolea, waingizaji na wafanyabiashara wa mbolea, watafiti, wanazuoni, taasisi za fedha, wadau wa maendeleo, wataalam wa kilimo na wakulima.
Katika kongamano hilo, washiriki watajadili na kuazimia masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Tasnia ya Mbolea na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.
