TFRA Yawataka Wakulima Mkoani Simiyu Kubadilika na Kuzingatia Kanuni Bora za Kilimo

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo, amewataka wakulima Mkoa wa Simiyu, kubadilika na kuanza kutumia mbinu bora za kilimo zikiwemo matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao yao.
Dkt. Diallo ametoa wito huo nyakati tofauti tarehe 12 na 13 Juni 2025, alipokuwa akizungumza na wakulima wa vyama vya msingi vya Ushirika na wakulima wa mazao ya Pamba na Mahindi wa wilaya za Itilima, Meatu na Maswa Mkoani Simiyu wakati wa ziara ya bodi na menejimenti ya TFRA iliyolenga kuhamasisha matumizi ya mbolea mkoani humo.
Akisisitiza umuhimu wa matumizi ya mbolea, Dkt. Diallo ameeleza kuwa, matumizi sahihi ya mbolea yatawafanya wakulima kuongeza uzalishaji na kulima eneo dogo la ardhi na hivyo kupunguza migogoro ya ardhi inayotokana na uhitaji wa mashamba makubwa wakati huohuo uzalishaji wake kutokuwa wa kuridhisha.
“Mkulima anaweza kulima ekari tatu tu na kufanikisha mahitaji yake ya chakula na kipato badala ya kulima maeneo makubwa bila tija,” anasema Dkt. Diallo.
Aidha, Dkt. Diallo ameeleza kuongezeka kwa kipato kwenye kaya zao kutapunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini na kufanya kazi zisizokuwa na tija na kuwaingiza katika makundi yasiyofaa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa TFRA, Bi. Elizabeth Bolle, ameeleza kuwa, lengo la ziara hiyo ni kuhamasisha matumizi ya mbolea ili kuongeza tija kwa wakulima pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili ili zitatuliwe kwa wakati na kuwafanya wakulima kuinua uchumi wao.
Naye, Mkaguzi wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Bw. Daniel Bariyanka, amewahimiza wakulima kuwatumia wataalam waliopo katika maeneo yao, ikiwemo washauri wa kilimo wa mpango wa BBT, ili wapewe elimu ya kanuni bora za kilimo cha pamba na mazao mengine.
“Bei ya pamba kwa sasa ni nzuri ukilinganisha na nchi jirani, lakini ili kufikia masoko ya uhakika na kupata faida kubwa, ni lazima tulime kwa tija na kutumia mbolea,” amesema Bariyanka.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao na bodi katika kijiji cha Bubalabujiga wilayani Itilima mkulima, Leticia Matanga, ameishukuru Bodi ya Mamlaka kwa kupeleka elimu hiyo muhimu na kuiomba iendelee kutoa elimu na kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea ili kubadilisha maisha yao.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukilima pamba bila kutumia mbolea na kuvuna kilo 250 kwa ekari moja, lakini leo tumejifunza kuwa, tukitumia mbolea tunaweza kuvuna zaidi ya kilo 1,000. Vilevile, tumeelezwa kuwa, mahindi tunayovuna gunia 5 hadi 7 kwa ekari yanaweza kufikia gunia 30 hadi 35 tukitumia mbolea," alisema Matanga.
Wakulima wa Wilaya ya Itilima waliiomba Serikali kupitia TFRA na wadau wengine wa kilimo kuendelea kutoa elimu endelevu kuhusu matumizi bora ya mbolea pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mbolea katika maeneo yao kwa wakati na kwa bei nafuu.
“Tunaomba elimu hii iendelee kutolewa mara kwa mara, na mawakala wasogezwe karibu na maeneo yetu ili tuweze kupata mbolea kwa urahisi.