Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

Announcements

TAARIFA KWA UMMA: BEI ELEKEZI ZA MBOLEA (DAP, UREA, CAN NA SA)


1.Utangulizi


Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Aurhority - TFRA) kwa niaba ya Wizara ya Kilimo ina jukumu la kutoa bei elekezi ya mbolea kwa wauzaji wa mbolea wa jumla na rejareja ambapo mbolea hizo zinatakiwa kuuzwa kwa bei hiyo au chini yake. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya Mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 (The Fertilizer (Amendment) Regulations, 2017).


Kutokana na hali ya kupanda kusiko kwa kawaida kwa bei za mbolea katika soko la dunia, Serikali kupitia Waziri wa Kilimo ilisitisha matumizi ya Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja na upangaji wa bei elekezi mwezi Julai, 2021 ili kuruhusu ushindani katika biashara ya mbolea kwa matarajio kuwa bei za mbolea zitakuwa himilivu kwa kuwa kila kampuni itafanya jitihada za kuagiza mbolea kutoka kwenye vyanzo vyenye bei nafuu na kuongeza upatikanaji wa mbolea kwa wakulima nchini.


Aidha, kufuatia changamoto ya baadhi ya makampuni kupandisha bei za mbolea bila sababu za msingi na kusababisha usumbufu kwa wakulima; Serikali imeweka utaratibu shirikishi wa kupanga bei elekezi kwa mbolea za DAP, UREA,CAN na SA. Hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea kwa kushirikisha Makampuni yanayoingiza mbolea nchini imepanga viwango vya bei za rejareja kwa mbolea hizo kwa uzani wa kilo 50, 25 na 5 katika kila kituo cha mauzo kuanzia tarehe 21 Machi, 2022. Lengo la kufanya hivyo ni kuondoa uwezekano wa wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia changamoto zilizopo kwenye soko la dunia kujinufaisha kwa kupandisha bei kiholela.


Endapo kutakuwa na changamoto kwa baadhi ya sehemu ambapo bei elekezi itakuwa haiakisi hali halisi; inapendekezwa Kamati za pembejeo ngazi ya mkoa/wilaya kukaa na wafanyabiashara wa eneo husika na kurekebisha bei hizo ili ziendane na hali halisi kwa kuzingatia jiografia na miundombinu ya eneo husika.


Ni muhimu kwa Mamlaka zote husika katika ngazi za Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuhakikisha kuwa kila duka la pembejeo linabandika bei elekezi sehemu zinazoonekana kwa urahisi kwa wanunuzi. Pia ni vema mamlaka hizo kusimamia bei ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa bei elekezi na upatikanaji wa mbolea kwa wakulima katika maeneo husika.

2.HitimishoIli kuhakikisha kuwa changamoto iliyojitoza ya upandishaji holela wa bei za mbolea haijitokezi tena, kuwawezesha wakulima kupata mbolea kwa bei himilivu kulingana na hali halisi ya soko na kuimarisha uzalishaji wa mazao;

i) Wauzaji wa mbolea zenye bei elekezi wahakikishe wanazingatia bei zilizopangwa na Serikali na wale wote watakaokiuka watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni ya kufanya biashara ya mbolea;

ii) Kamati za pembejeo za Mikoa na Wilaya zifuatilie hali ya upatikanaji wa mbolea katika maeneo yao na uzingatiaji wa bei elekezi ya mbolea na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaoonekana kukiuka taratibu na maagizo haya;

iii) Wakulima wazingatie Kanuni bora za Kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya pembejeo za Kilimo.

iv) Wataalam wa Kilimo na wadau mbalimbali waendelee kuhamasisha na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea ikiwemo kupima afya ya udongo.

Dkt. Stephan E. Ngailo

MKURUGENZI MTENDAJI.

Machi 21, 2022

Tanzania Census 2022