MRADI WA KUIMARISHA UPATIKANAJI NA KUONGEZA MATUMIZI YA MBOLEA NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilianzisha na kutekeleza mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System-BPS) kwa lengo la kuimarisha upatikanaji na kuongeza matumizi ya mbolea kwa wakulima. Aidha, uanzishwaji wa mfumo huu ulikusudia kutatua changamoto ya bei kubwa za mbolea zilizokuwepo katika soko hapa nchini. Kwa zaidi ya asilimia 90 ya mbolea zote zinazotumika hapa nchini huagizwa kutoka nje ya nchi. Kila mwagizaji wa mbolea (importer) alikuwa akiagiza mbolea kulingana na uwezo wake, hivyo kufanya bei ya mbolea kuwa juu. Kwa kuwa uzalishaji wa mazao na tija unategemea matumizi ya pembejeo hususan mbolea, Wizara ya Kilimo ilibuni mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja ulioleta matokeo chanya ya kupunguza bei ya mbolea kwa mkulima kwa kati ya asilimia 10 hadi 40 na kuongeza matumizi ya mbolea kutoka tani 302,450 msimu 2015/16 hadi tani 435,178.48 kwa msimu 2017/18 (ongezeko la asilimia 69). Kuongezeka kwa matumizi ya mbolea kumechangia vilevile kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hususan mahindi na mpunga kwa nchi nzima. Aidha, kupitia mfumo wa PBS serikali iliweza kupanga na kusimamia bei elekezi za mbolea ambazo zilimwezesha mkulima mdogo kumudu kununua mbolea na kuitumia.

Kutokana na mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja, Serikali imeokoa jumla ya shilingi bilioni 20.5 (saving ya DAP bilioni 7.8 na urea bilioni 12.7) kama punguzo linalotokana na ununuzi wa mbolea kwa pamoja (economies of scale) ambapo bila BPS serikali ingetumia fedha hizo kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili kupunguza bei ya mbolea.

Mambo mengine yaliyofanywa na serikali ni pamoja na;

Kuondoa tozo mbalimbali zilizokuwa zikitozwa na taasisi mbalimbali kwa mbolea zilizokuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi kama vile Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Nguvu za Atomiki (Tanzania Atomic Energy Commision), Mkemia Mkuu wa Serikali, Wakala wa Vipimo (WMA), kufuta ada ya leseni za mbolea na ada za usajili wa mbolea ambako zilichangia kupunguza bei ya mbolea kwa mkulima.  

Kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiashara wa mbolea na wakulima kwa maana ya sera, sheria na kanuni zilizofanya tasnia ya mbolea kuwa na mvuto na ufanisi mkubwa katika utekelezaji wake katika mnyororo mzima wa thamani. Mapitio ya sheria, kanuni na taratibu yaliyofanyika ni pamoja na; kupunguza muda wa kusajili mbolea; kutoka miaka mitatu hadi miezi sita tu. Sambamba na hilo serikali iliondoa sharti  la kufanya majaribio kwa mbolea zenye kuongezewa vitubisho kulingana na mahitaji ya zao au udongo (ferilizer blends) kutoka miaka mitatu hadi siku 2-5 tu. Kupunguza gharama za utafiti wa mbolea mpya (new molecule) kwa asilimia 70. Hali hii imeongeza wafanyabiashara wa mbolea kutoka 420 hadi 2,500 na hivyo kuongeza vituo vya mauzo na mawakala wa mbolea nchini.

Kusimamia kwa dhati udhibiti wa ubora wa mbolea hapa nchini hivyo kutokomeza kwa asilimia 100 mbolea feki (counterfeit fertilizer). Hali hii imekuwa na matokeo chanya ya kumwepusha mkulima kupata hasara ya kutumia mbolea isiyokuwa sahihi. Kwa sasa serikali inaendelea kutoa elimu kwa wauzaji wa mbolea isiyokidhi viwango kutokana na uhifadhi/utunzaji duni (poor handling and storage) katika maduka ya Mawakala.

Contact Details

TANZANIA FERTILIZER REGULATORY AUTHORITY
Mandela Road, Temeke Veterinary.
Ministry of Livestock and Fisheries
Former PADEP Building
P.O Box 46238,
Dar Es Salaam,
Tanzania
Tel: +255 22-2862595
Mobile: +255 710107631
E-mail: info@tfra.go.tz