WAZIRI WA KILIMO ATANGAZA BEI ELEKEZI YA MBOLEA AINA YA DAP NA UREA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA KILIMO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

BEI ELEKEZI KWA MBOLEA YA KUPANDIA (DAP) NA YA KUKUZIA (UREA) KWA MSIMU WA KILIMO 2018/2019

  1. UTANGULIZI

Tanzania ni moja ya nchi kusini mwa jangwa la Sahara ambayo imeongeza matumizi ya mbolea kwa kasi kubwa. Hii ni kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement System), kufuta tozo mbalimbali za mbolea, kusimamia utaratibu wa usafirishaji wa mbolea na kuweka bei elekezi ya mbolea kwa mkulima. Juhudi zote hizi zimefanya bei ya mbolea kupungua na hivyo kufanya wakulima wawe na uwezo wa kununua mbolea zaidi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 4(1)(u) cha Sheria ya Mbolea ya mwaka 2009 na Kanuni ya 56 ya Kanuni za Mbolea (2011) na marekebisho yake ya mwaka 2017 (The Fertilizer (Amendment) Regulations, 2017) na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) Na. 50 la Februari 17, 2017, mbolea aina zote zinatakiwa kuuzwa kwa bei iliyopangwa na Serikali.

Mbolea zinazotumika hapa Tanzania kwa sasa ni pamoja na Minjingu, TSP, DAP, Urea, NPK, CAN na SA. Aidha, mbolea zingine zinazotumika ni zile za asili kama mboji na samadi. Kwa sasa bei elekezi itakayotangazwa ni kwa mbolea zinazoagizwa kupitia zabuni za ushindani za mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (BPS) ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na ya kukuzia (Urea).

  1. Gharama za ununuzi na uingizaji wa mbolea kutoka nje na usambazaji nchini

Katika kutengeneza mjengeko wa bei, gharama ya kwanza ni bei ya ununuzi na usafirishaji wa mbolea baharini pamoja na gharama zingine hususan tozo za Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Bei elekezi za mbolea zinategemea umbali wa sehemu inakopelekwa. Kwa sasa, usafirishaji wa mbolea ndani ya nchi unatumia zaidi barabara. Maeneo yote itakapopelekwa mbolea yana umbali kati ya kilometa 1 hadi kilometa 1,600 kutoka bandari ya Dar es salaam ambako mbolea huingilia kutoka nchi inakotengenezwa/kununuliwa.

Kwa Wastani, gharama ya kusafirisha mfuko mmoja wa mbolea kwa barabara kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi makao makuu ya Halmashauri kwa barabara ni Sh. 5,500/= kwa kilometa 1,000. Gharama hii hupanda na kushuka kutegemeana na hali ya barabara na hali ya hewa (masika au kiangazi).

  1. Bei elekezi: Mwenendo, mchanganuo na ushauri
  • Mwenendo wa bei elekezi katika soko la Dunia

Mnamo Julai, 2018 Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ilifungua zabuni kwa ajili ya kuingiza tani 30,000 za mbolea ya kukuzia (Urea) na tani 35,000 za mbolea ya kupandia (DAP). Bei ya chanzo kwa mujibu wa mzabuni aliyeshinda ilikuwa US$ 290 (mbolea ya Urea) na US$ 370 kwa mbolea ya DAP kwa tani moja. Ikilinganishwa na bei za chanzo zilizokuwepo Julai, 2017 (US$ 307 kwa DAP na US$ 193 kwa Urea), kuna ongezeko la bei ya chanzo kwa asilimia 21 (DAP) na asilimia 53 (Urea). Kutokana na ongezeko hili la bei ya chanzo, bei elekezi ya mkulima itaongezeka kwa aina zote mbili za mbolea.

Pamoja na ongezeko hilo, bei hizi zingekuwa kubwa zaidi kama mbolea ingeingia nchini bila kupitia mfumo wa zabuni kwa ushindani wa BPS. Siku ya ufunguzi wa zabuni ya Urea (Julai 11, 2018) bei katika soko la Dunia ilikuwa US$ 310 (sawa na asilimia 6% zaidi ya bei ya zabuni). Siku ya ufunguzi wa zabuni ya DAP (Julai 18, 2018) bei katika soko la Dunia ilikuwa US$ 430 (sawa na asilimia 14% zaidi ya bei ya zabuni).

  • Mchanganuo wa bei elekezi na Maelekezo kwa Tawala za Mikoa

Kwa muktadha huo, bei elekezi ya mbolea aina ya DAP kwa mikoa ya Kanda ya Mashariki, Kati, Kusini na Kaskazini zitakuwa kati ya Sh. 56,100/= na 67,600/=. Aidha, bei elekezi ya mbolea aina ya Urea kwa mikoa ya Kanda hizo itakuwa kati ya Sh. 48,500/= na 59,300/=. Kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi, Nyanda za Juu Kusini, na Ziwa, bei elekezi kwa mbolea aina ya DAP itakuwa kati ya Sh. 60,700/= na 70,600/=. Bei ya mbolea aina ya Urea kwa mikoa hiyo itakuwa kati ya Sh. 52,900/= na 62,300/=. Bei hizi zitaanza kutumika rasmi tarehe 22 Septemba, 2018 na zitaendelea kutumika hadi pale itakapotangazwa bei nyingine.

Endapo kutakuwa na tofauti ya gharama za usafirishaji kwa baadhi ya sehemu katika maeneo yenu ambayo yatakuwa hayaendani na bei elekezi, maelekezo ya suala hili nilishayatoa kwa Wakuu wa Mikoa/Wilaya kuwapa Mamlaka ya kukaa na Kamati za pembejeo na kurekebisha bei elekezi ili ziendane na hali halisi kwa kuzingatia jiografia ya eneo husika.

Aidha, ili kumwezesha mkulima mdogo kupata mbolea hizi zikiwa katika hali ya ubora unaokubalika, Wizara imetoa pia bei za mbolea kwa uzani wa kilo 25, 10 na 5. Wakulima wanashauriwa kununua mbolea katika mifuko maalum. Kisheria ni kosa kuuza mbolea kwa bei ya juu kuliko iliyotangazwa kwa nia ya kujiongezea kipato.

  • Ushauri kuhusu namna ya kupata mbolea kwa bei nafuu zaidi

Kutokana na kurahisishwa kwa taratibu za uingizaji wa mbolea nchini na pia kutokana na changamoto ya kupata fedha taslimu za kununua mbolea wakati muafaka, wakulima wadogo kupitia vyama vya msingi (AMCOS – Agricultural Marketing Cooperative Societies) na vyama vikuu vya ushirika (Co-operative Unions) wanashauriwa kupata dhamana ya Benki (Bank guarantee) ili ziwawezeshe kuleta mahitaji yao ya mbolea kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili iwafanyie utaratibu wa kuwaagizia mbolea kwa pamoja.

Endapo watatumia utaratibu huo, Wizara yangu iko tayari kuzungumza na mashirika ya Reli na wasimamizi wa maghala ya Serikali ili mbolea hiyo isafirishwe na kuhifadhiwa kwa gharama nafuu ili isubiri msimu wa matumizi. Kwa kufanya hivi, wakulima wataondokana na changamoto ya uhaba wa mbolea au wakulima kushindwa kuinunua kutokana na kuuzwa kwa bei kubwa.

  1. Hitimisho

Nitoe wito kwa wataalam na wadau wa kilimo kutoa ushirikiano wa dhati katika kuwaelekeza wakulima matumizi sahihi ya mbolea ili kufikia lengo la kujitosheleza kwa chakula kwa Taifa sambamba na kuongeza kipato cha mkulima. Aidha, nitoe wito kwa Mamlaka zote katika ngazi za mikoa, Wilaya na Halmashauri kutoa ushirikiano katika jambo hili ili mkulima aweze kutumia fursa hii kubadilisha maisha yake kupitia kilimo.

Asanteni sana kwa kunisikiliza

Download/Pakua: Bei elekezi ya mbolea aina ya Urea kuanzia Septemba 22, 2018

Download/Pakua: Bei elekezi ya mbolea aina ya DAP kuanzia septemba 22, 2018

 

MHE. DKT. CHARLES JOHN TIZEBA (MB)

WAZIRI WA KILIMO.

Septemba 18, 2018

Contact Details

TANZANIA FERTILIZER REGULATORY AUTHORITY
Mandela Road, Temeke Veterinary.
Ministry of Livestock and Fisheries
Former PADEP Building
P.O Box 46238,
Dar Es Salaam,
Tanzania
Tel: +255 22-2862595
Mobile: +255 710107631
E-mail: info@tfra.go.tz